Historia ya vita vya Syria na ukuaji wa kundi la IS.
Ingawa uwepo wa kundi la IS ulisukuma jumuiya za kimataifa kuingilia mzozo wa Syria, kundi hilo lilijiingiza kwenye mzozo huo baadae. DW inaangazia namna gani vita hivyo vimetoa mwanya kwa kundi hilo kujitanua.
Athari ya vuguvugu la "mapinduzi ya Uarabuni"
Mnamo mwaka 2011, wakati serikali iliposhindwa kutimiza matarajio.Makumi kwa maelfu ya Wasyria waliandamana mitaani kupinga rushwa, ukosefu wa ajira na kupanda kwa bei za vyakula. Serikali ya Syria ilisambaratisha maandamano hayo kwa silaha za moto na kusababisha mauaji ya watu 400, mwezi Mei.
Wito wa kulaani vita bila ya muafaka
Katika ushawishi wa Mataifa ya Magharibi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani hatua za ukandamizaji. Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani waliweka vikwazo vya silaha, kuzuia mali na viza katika miezi iliyofuatia. Huku wakiungwa mkono na Umoja wa nchi za Kiarabu, walitoa mwito zaidi wa kuondoka kwa rais wa Syria. Lakini si wanachama wote wa Umoja wa Mataifa walikuabaliana na mwito huo.
Assad akataa kuachia madaraka
Bashar al-Assad - ambaye amekuwa madarakani tangu kifo cha baba yake mwaka 2000 - ameshuhudia kufifia kwa hadhi yake kutokana na kuendelea kwa machafuko. Anakataa kuhitimisha muda mrefu wa utawala utakaoruhusu ufuatiliaji na kuhojiwa. Urusi aliye mshirika wake, ameendelea kusambaza silaha na kupiga kura ya turufu mara kadhaa kwa maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Syria.
Upinzani wajipanga
Hadi mwishoni mwa mwaka, makundi ya haki za binaadamu na Umoja wa Mataifa walikuwa na ushahidi kuhusu kuvunjwa kwa haki za binaadamu. Raia na waliotengwa na jeshi walianza kujipanga kupambana na majeshi ya serikali, ambayo yalikuwa yakiwalenga wapinzani. Zaidi ya wapiganaji 5,000 wameuwawa katika mapigano. Ilichukua miezi mingine sita kabla Umoja wa Mataifa haujakiri kuwepo kwa vita nchini Syria.
Uingiliaji kutoka nje
Mwezi Septemba 2012, Iran ilithibitisha uwepo wa wapiganaji wake nchini Syria- jambo ambalo kwa muda mrefu Damascus ililikataa. Uwepo wa majeshi ya washirika wa Syria uliwafanya Marekani na Mataifa ya Magharibi kusita kuingilia mgogoro huo. Marekani ambayo bado ilikuwa na machungu ya kuingilia kati mzozo wa Afghanistan na Iraq, iliona suluhisho pekee ni mazungumzo.
Kuyakimbia machafuko
Wakati vifo vikikaribia 100,000, idadi ya wakimbizi katika mataifa jirani ya Uturuki na Jordan ilifkia Milioni moja. Idadi hiyo iliongezeka mara mbili hadi Septemba 2013. Mataifa ya Magharibi na ya Kiarabu yameshuhudia kushindwa kwa hatua zote za kuwa na serikali ya mpito , huku mapigano yakisambaa Uturuki na Lebanon. Wana hofu kwamba Assad ataendelea kubaki madarakani kwa njia zozote.
Hakuna Umoja dhidi ya Assad
Assad amekuwa akidai kupambana na magaidi. Lakini haikuwa hivyo hadi mwaka wa pili wa vita ambapo Jeshi huru la Syria liligawanyika na kujulikana kuhusisha wapiganaji wa itikadi kali. Kundi la Al Nusra Front lilikiri kuwa na mafungamano na na lile la Al-Qaeda na baadae kuugawa zaidi upinzani.
Kutoka matumizi ya nguvu hadi silaha za kemikali
Mwezi Juni 2013, Ikulu ya Marekani ilisema inao ushahidi kwamba Assad amekuwa akitumia gesi ya sumu dhidi ya raia- ripoti ambayo baadae iliungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Ugunduzi huo ulimsukuma rais Barack Obama na viongozi wengine wa mataifa ya Magharibi kuzingatia matumizi ya nguvu za kijeshi. Hata hivyo pendekezo la Urusi la kuondoa silaha za kemikali lilishinda
Kundi la Dola la Kiislamu laibuka
Ripoti za kundi jipya la Jihadi linalojiita Dola la Kiislamu ISIL zilienea katika wiki za mwisho za 2013. Wakichukua udhibiti kaskazini mwa Syria na Iraq, kundi hilo lilichochea mapigano miongoni mwa upinzani , kufikia mapema 2014 baadhi yao 500 walikuwa wameuawa. Kuibuka kwa IS ambako hakukutarajiwa kuliwaleta pamoja Marekani, Ufaransa na Saudi Arabia pamoja na mataifa mengine katika vita hiyo.