1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heiligendamm, Ujerumani. Waandamanaji kutoweza kufika karibu na mkutano.

2 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBvm

Waandamanaji wanaopinga utandawazi hawataweza kufika karibu na eneo la mkutano wa kundi la mataifa yenye utajiri mkubwa wa viwanda G8 mjini Heiligendamm baada ya mahakama moja nchini Ujerumani kubadilisha maamuzi yake ya hapo awali.

Eneo lililotengwa na polisi kwa ajili ya maandamano pia limeongezwa kutoka kilometa sita hadi 12.

Jaji aliyesikiliza kesi hiyo mjini Greifswald amesema kuwa kuna wasi wasi wa usalama kutokana na njia nyembamba kuelekea katika eneo hilo la mkutano, ambalo limefungwa kwa ukuta wa seng’enge.

Msemaji wa mahakama hiyo amesema maandamanao yanayotarajiwa hapo Juni 7 yangesababisha kufunga njia zote. Kiasi cha maafisa usalama 16,000 watakuwapo katika mji huo ulioko pwani wakati wa mkutano utakaoanza Juni 6 hadi 8 ili kushughulika na waandamanaji wanaokadiriwa kufikia laki moja.