1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya rais wa Benki ya Dunia Wolfowitz kujulikana leo

15 Mei 2007

Jopo la wakurugenzi wa Benki ya dunia limesema kuwa rais wa benki hiyo Paul Wolfowitz alivunja sheria za taasisi hiyo kwa kumwongezea mpenzi wake mshahara kwa kiwango kikubwa.

https://p.dw.com/p/CHEM
Rais wa Benki ya Dunia Paul Wolfowitz
Rais wa Benki ya Dunia Paul WolfowitzPicha: AP

Bwana Wolfowizt sasa anasubiri uamuzi wa bodi kamili ya wakurugenzi hao juu ya mustakabal wake.

Wakurugenzi hao wamesema sasa bodi kamili ya benki yote itaamua iwapo bwana Wolfowitz bado ana uwezo wa kuiongoza benki hiyo.

Bwana Wolfowitz anatarajiwa kusimama mbele ya bodi hiyo ya wakurugenzi wote 24 mjini Washington.Bodi hiyo ina mamlaka ya kumfukuza kazi rais huyo wa benki, kumwonya ama kutoa ripoti juu ya kutokuwa na imani na uongozi wake.

Bwana Wolfowitz anadaiwa kusababisha utatanishi katika taratibu za benki ya dunia.Jopo la wakurugenzi limetahadharisha juu ya kuwapo mgogoro wa uongozi katika benki hiyo.Wanajopo wamesema kuwa bwana Wolfowitz alikeuka sheria za benki kwa kumwongezea mpenzi wake malipo ya kiwango kikubwa.

Wakati wakurugenzi wote 24 wa bodi ya benki ya dunia wanatarajiwa kutafakari iwapo bwana Wolfowitz bado ana uwezo wa kuendelea kuiongoza benki hiyo kwa uthabiti , rais huyo mwenyewe amesema kuwa bado anaweza kuendelea kutekeleza majukumu ya taasisi hiyo.

Kashfa ya bwana Wolfowitz imezigawanya nchi 185 wanachama wa benki hiyo. Katika upande mmoja Marekani inamwuunga mkono na katika upande mwingine serikali kadhaa za nchi za Ulaya zinataka Wolfowitz aachishwe kazi.

Hatima yake itajulikana baada ya kiako cha bodi ya wakuregenzi wote 24 wa benki ya dunia leo.

Wolfowitz alihusika moja kwa moja katika mpango wa malipo ya dola laki mbili zilitotolewa kwa mpenzi wake bibi Riza alipohamishiwa kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani mnamo mwaka 2005 ili kuepusha mgongano na mkubwa wake mpya wa kazi.

Lakini jopo la wakurugenzi limesema katika ripoti yake kwamba uhusiano baina ya bwana Wolfowitz na bibi Riza ulivuka hatua ya kuepusha kinachoitwa mgongano.Jopo la wakurugenzi sasa limetoa ushauri kwa bodi kamili ya benki kutafakari iwapo bwana Wolfowitz bado ana uwezo wa kuendela kuiongoza benki.

Pamoja na mambo mengine bwana Wolfowitz analaumiwa kwa kuweka mbele maslahi yake binafsi badala ya taratibu za benki

Hatahivyo bwana Wolfowitz bado anaungwa mkono na rais G. Bush . Rais Bush amesema kuwa Wolfowitz pia ana haki ya kujieleza.

Gazeti maaruf Financial Times limeripoti kuwa Marekani inakusudia kuitisha kikao cha dharura cha mawaziri wa kundi la nchi saba ili kuwashawishi mawaziri hao wamruhusu bwana Wolfowitz aendelee na kazi yake. Afisa mmoja wa Marekani ambae hakutaka kutajwa jina , amethibitisha habari za gazeti hilo.

Mkasa wa Wolfowitz unatishia kuathiri shughuli za benki za kutoa mikopo na kusaidia juhudi za mandeleo na pia unatishia kuathiri kampeni ya kupiga vita rushwa.

Wakati dunia inasubiri kujua hatima ya bwana Wolfowitz tayari kuna uvumi juu ya watu watakaochukua nafasi yake ikiwa pamoja na bwana Robert Zoellick aliekuwa mwakilishi wa biashara wa Marekani. Mwengine ni Mohammed el Erian wa Misri ambae sasa yupo chuo kikuu cha Havard . Jina jingine ni bwana Kemal Davis wa Uturuki ambae sasa ni mkuu wa shirika la maendeleo la Umoja wa mataifa.

A.M