1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hata Gaddafi akishinda, hautakuwa mwisho wa vita

14 Machi 2011

Wakati kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, akiendelea kupanda ushindi wa kijeshi dhidi ya waasi, wafuatiliaji wa mzozo wa nchi hiyo wanasema ushindi huu unawarudisha nyuma waasi lakini hautavimaliza vita.

https://p.dw.com/p/10Ytq
Mpambanaji wa Libya dhidi ya Gaddafi
Mpambanaji wa Libya dhidi ya GaddafiPicha: dapd

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa uwezekano wa majeshi ya Kanali Gaddafi kupata ushindi kamili katika mapambano hayo upo, kwani majeshi hayo yanatumia mashambulizi ya angani pamoja na silaha nyingine nzito, ambazo waasi hawana, na hilo linawafanya wanajeshi wa Gaddafi kuonekana wakiimarika dhidi ya waasi.

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini Marekani, James Clapper, akizungumza mbele la Baraza la Seneti alisema kuwa, kutokana na ubora wa vifaa na nidhamu waliyonayo wanajeshi wa Gaddafi kuliko waasi, hatimaye utawala huo utafanikiwa kuuzima uasi.

Libyen Demonstration gegen Muammar Gaddafi in Bengasi Flagge
Libyan women wear pre-Gadhafi flags as they protest to demand the resignation of Libyan leader Moammar Gadhafi during a demonstration in Benghazi, eastern Libya, Wednesday, March 9, 2011. (Foto:Kevin Frayer/AP/dapd)Picha: dapd

Lakini wachambuzi wanasema kuwa, pamoja na ushindi atakaoupata Kanali Gaddafi, si kwamba ataweza kudhibiti nchi hiyo kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka 41 ya utawala wake.

Badala yake, miji ya mashariki kama vile Benghazi, ambao kihistoria umekuwa kitovu cha uasi dhidi ya utawala wa Gaddafi, itaendelea kupambana na udhibiti wa serikali.

Katika hatua hiyo, uwezekano ni mkubwa kwa upinzani huo kuendeshwa katika mtindo wa vita vya chini kwa chini. Wapiganaji hao wataweza kuhifadhiwa na wakaazi wa miji hiyo, ambao watakuwa wameathiriwa na harakati za vikosi vya serikali dhidi ya waasi.

Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: dapd

Hali kadhalika, watahifadhiwa na raia waliokuwa wakiandamana kuipinga. Pia wachambuzi hao wanaona kuwa uwezekano mkubwa wa kupata misaada ya kijeshi kutoka nje.

Vile vile, vongozi wa vita hivyo vya chini kwa chini wataweza kutumia mwanya wa mpasuko katika utawala wa Gaddafi, hususan kwa wale wasaidizi wake wakiwemo maafisa wa juu wa jeshi, viongozi wa kikabila pamoja na maafisa wengine wa serikali waliotangaza kumtupa mkono na kujiunga na uasi.

Na kwa upande mwengine, Kanali Gaddafi atakuwa akikabailiwa na vikwazo vya jumuiya ya kimataifa vitakavyomzuia kuweza kupata fedha, silaha na kusafiri nje.

Profesa Yezid Sayigh, ambaye ni mkufunzi wa katika Idara ya Mafunzo ya Kivita kwenye chuo cha King mjini London, anasema kuwa iwapo Kanali Gaddafi atafanikiwa kudhibiti tena nchi, basi itakuwa katika sura mpya ya nchi iliyogawika kikabila na kieneo.

Profesa Sayigh anasema kuwa, sehemu kubwa ya wananchi hawatakuwa tayari kumpatia Kanali Gaddafi taarifa za kiintelejensia ambazo angependa kuzipata, ili kuweza kukabiliana na wanamgambo hao watakaoendesha vita vya chini kwa chini.

Kwa upande wake, Graham Cundy, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijeshi katika kampuni ya ushauri wa mambo ya kiulinzi na usalama ya Diligence iliyoko mjini London, anasema katika eneo la mashariki mwa Libya, hakuna uhaba wa risasi na silaha. Mtaalamu huyo anaonya kuwa, wakaazi wa mijini wataweza kutoa maficho kwa wanamgambo watakaoendesha vita hivyo.

Cundy, ambaye ni ofisa wa zamani katika jeshi la Uingereza na mwenye uzoefu wa muda mrefu wa vita vya chini kwa chini nchini Afghanistan,ameongeza kuwa, waasi hao wa mashariki wana kila kitu cha kuwafanya waendelee na vita hivyo dhidi ya utawala wa Gaddafi.

Wataalamu wa masuala ya kivita wanasema vita vya chini kwa chini dhidi ya serikali iliyoko madarakani vinahitaji maeneo salama, ambako wanamgambo wataweza kujijenga upya, kukusanya nguvu na kupanga mashambulizi.

Mfano wa maeneo hayo ni kama milimani, maeneo yaliyotekwa, maeneo ya mbali vijijini yasiyofikika kwa urahisi, nchi jirani zitakazowaunga mkono au katika miji ambako kunaweza kuwa maficho mazuri kwao.

Kwa Libya, ambayo ukubwa wake ni mara mbili na nusu zaidi ya Ufaraansa, haina milima na maeneo mengi ya mbali huenda yakajikuta yakidhibitiwa na makundi ambayo serikali itakuwa na mashaka kushirikiana nayo.

Kwa maana hiyo, anasema Shashank Joshi, kutoka taasisi ya kijeshi ya Royal United Service nchini Uingereza, uwezekano ni mkubwa katika miji ya mashariki kuwa na maeneo ambayo yatakuwa ngome ya waasi watakaoshindwa na majeshi ya serikali.

Ametolea mfano mji wa Zawiyah, ambao majeshi ya serikali yamefanikiwa kuutwaa lakini baada ya siku kadhaa za mapambano na upinzani wa waasi.

Hata hivyo, Noman Benotman ambaye huko nyuma katika miaka ya 1990 alipambana na utawala wa Gaddafi kama mwanamgambo wa Kiislam, anasema wanachotakiwa kukifanya hivi sasa waasi wa mashariki, ni kujikusanya upya.

Anasema, ingawa tatizo ni kwa waasi hao kutokuwa na uzoefu, lakini iwapo wataweza kujiimarisha, basi wataweza kuendesha mapambano ya chini kwa chini yatakayokuwa mateso makubwa kwa majeshi ya Kanali Gaddafi.

Mwandishi: Aboubakary Liongo/Reuters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo