1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamburg yaibwaga Hoffenheim

Bruce Amani
27 Novemba 2017

Kocha Markus Gisdol aliisaidia SV Hamburg kupata ushindi rahisi dhidi ya timu yake ya zamani Hoffenheim kwa kuwazaba mabao matatu kwa sifuri

https://p.dw.com/p/2oKqJ
Deutschland Hamburger SV vs. TSG Hoffenheim - Bundesliga Eigentor
Picha: picture-alliance/dpa/D. Reinhardt

Ushindi huo wa nne msimu huu kwenye ligi, umewaondoa Hamburg katika eneo hatari la kushushwa ngazi na kupanda hadi nafasi ya 15. Na Gisdol, ambaye alikuwa kocha wa Hoffenheim kuanzia 2013 – 2015 amelala na tabasamu kubwa baada ya kumpiku katika mbinu za kiufundi kocha anayesifika sana Jualian Nagelsmann mwenye umri wa miaka 30. Christian Mathenia ni mlinda mlango wa Hamburg "Tumeona katika wiki chache zilizopita. Hatukuwahi kucheza soka mbaya. Siku zote niliona kama tulicheza vyema hata kama tulipoteza baadhi ya mechi hizo, lakini tulisema leo hatutaki kucheza kandanda la kuvutia bali tulitaka tu kupata pointi tatu hapa na tumefanya hivyo na tunajivunia sana kwa hilo".

Hoffenheim wameshuka hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, baada ya mechi 13 wakiwa na ushindi mmoja tu katika mechi zao saba za mwisho. Timu hiyo ya Nagelsmann ilitupwa nje ya Europa League wiki iliyopita.

Deutschland Hamburger SV vs. TSG Hoffenheim - Bundesliga
Hoffenheim walionekana kuishiwa mbinuPicha: picture-alliance/dpa/D. Reinhardt

Katika mchuano mwingine wa jana, washika mkia Cologne walizabwa mbili bila na Hertha Berlin. Kocha Peter Stoeger anakabiliwa na shinikizo, lakini amepewa uungwaji mkono na viongozi wa Cologne mpaka sasa, hasa kwa sababu bado inafanya vyema katika mashindano mengine ya Ujerumani na Europa League. Msikilize Stoeger "Kwa vijana wangu wlaiocheza leo lazima niseme, ilikuwa kazi nzuri. Walijituma sawasawa. Hakukuwa na suluhisho bora. Ni hali ngumu. Unapojikuta katika hali ya yenye mapungufu, inakuwa rahisi kufanya makossa na hilo limetokea kwetu na wakatuadhibu. Na kisha kuwa na Imani ya kuyabadilisha matokeo kama haujapata chochote kwa muda mrefu – hicho ni kibarua kigumu".

Ushindi wa Hertha uliwapandisha hadi nafasi ya 11. Habari kubwa ya wikiendi hata hivyo ilitokea katika uwanja wa Signal Iduna Park. Ilikuwa mojawapo ya mechi zilizokuwa zimesubiriwa kwa hamu msimu huu na kwa kweli ilitimiza hilo. Baada ya Borussia Dortmund kuongoza kwa mabao manne kwa sifuri katika kipindi cha kwanza dhidi ya watani wao wa jadi, Schalke walitoka nyuma na kufunga manne katika kipindi cha pili na kutoka sare.

Fußball Trainer Peter Bosz
Kocha Bosz anakabiliwa na shinikizoPicha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

Kocha wa BVB Peter Bosz aliingia katika mechi hii kwa hakika akihitaji ushindi, baada ya kukiri yeye mwenyewe kuwa kama timu yake ingeshindwa kufanya hivyo, huenda angepigwa kumbo ifikapo Jumapili asubuhi. Na kweli timu yake ilionekana kumuunga mkono kocha kwa kuanza kwa kasi na kushambulia mizinga langoni kwa Schalke. Lakini mambo yakaharibika katika kipindi cha pili walipozidiwa nguvu na Schalke, huku Pierre Emerick Aubameyang, akipewa kadi nyekundu. Kocha wa Schalke Domenico Tadesco alifanya mabadiliko katika dakika ya 25 kwa kumuingiza uwanjani kiungo Leon Goretzka, msikilize mchezaji huyo "Nadhani hatukuwa na bahati kabisa katika kipindi cha kwanza. Tulikuwa nyuma kwa mabao manne kwa sifuri, na kocha akageuka mara moja katika dakika ya 25 na kuniambia, anza kupasha misuli moto, baada ya dakika tano utaingia uwanjani. Na ndio nikaaza kupata tena nafasi ya kucheza tena na kuwa tayari kucheza wikendi hii inayokuja. Nilifurahi kucheza mechi hii. Tulianza kipindi cha pili kwa kasi na mwishowe sare ya 4-4 ikatosha. Ni ajabu sana!

Bosz hata hivyo ataendelea kuwa kocha angalau kwa sasa, baada ya Afisa Mkuu Mtendaji wa BVB Hans-Joachim Watzke kusema kuwa anamuunga mkono. Watzke amemtaka Bosz kukaza buti na kurekebisha mambo katika klabu hiyo ili watimize malengo yao ya msimu huu.

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund vs. FC Schalke 04
Kulizuka pata shika baada ya mechi kukamilikaPicha: picture-alliance/dpa/G. Kirchner

Nao viongozi wa ligi Bayern Munich ambao wana pointi 29, walicharazwa 2-1 na nambari nne kwenye ligi Borussia Moenchengladbach matokeo ambayo yalitia kikomo ushindi wao wa mechi tisa mfululizo katika mashindano yote tangu kocha Jupp Heynckes alipochukua usukani kutoka kwa Carlo Ancelotti. Gladbach sasa wamewaruka Dortmund na kupanda nafasi ya nne.

RB Leipzig waliwaruka Schalke na kusonga katika nafasi ya pili na pengo la pointi mbili, baada ya kuishinda Werder Bremen mbili sifuri, na sasa wako nyuma ya Bayern na pengo la pointi tatu tu, baada ya kuchezwa mechi 13. Ralph Hassenhutl ni kocha wa Leipzig "Werder walicheza vizuri leo. Walitufanyisha kazi ngumu kwetu kwa kucheza kwa ujasiri mkubwa. Wkanza tulidhani watacheza kwa kujilinda tu kumbe walitaka kucheza kwa kasi na ndio maana nadhani tulihitajika kufanya vyema ili kushinda mechi hii na bila shaka tulikuwa na nafasi kadhaa ambazo tungetumia lakini mwishowe, hizi ndio mechi baada ya Champions League ambazo tumeshinda mara kadhaa na zote zinafanana kiasi. Sio rahisi kucheza kwa dakika 90 dhidi ya timu kubwa katikati ya wiki na kisha kiakili uwe tayari kucheza wikendi dhidi ya mpinzani imara, nadhani tumefanya vyema". 

Wolfsburg ilifungwa mabao mawili kwa moja na Augsburg, wakati Freiburg ikiituliza Mainz mbili moja na kuondoka katika eneo la kushushwa ngazi. Bayer Leverkusen ilisonga hadi nafasi ya nafasi ya sita baada ya kuishinda Eintracht Frankfurt 1-0.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman