Hali ya wasiwasi yazidi Misri kufuatia shambulio la bomu Alexandria | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali ya wasiwasi yazidi Misri kufuatia shambulio la bomu Alexandria

Wasiwasi wa kuzuka machafuko ya kidini umeongezeka nchini Misri baada ya waandamanaji wa Kikristo wenye hasira kumvamia waziri mmoja kwa mawe, kutokana na shambulio la bomu katika Kanisa moja lililowaua watu 21

default

Wakristo wa madhehebu ya Coptic nchini Misri wakiandamana baada ya shambulio la bomu

Waandamanaji hao ni miongoni mwa mamia ya Wakristo wa madhehebu ya Coptic waliokuwa wamekusanyika ndani la milango mikuu ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Marko mjini Cairo, ambako kiongozi wa Kanisa hilo, Shenouda wa Tatu alikuwa anawapokea maafisa wanaokuja kumpa pole kutokana na shambulio hilo la bomu lililotokea Alexandria siku ya mwaka mpya lililowaua watu 21 na kuwajeruhi wengine 79.

Waandamanaji hao walimfukuza Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Misri, Osman Mohammed Osman hadi katika gari lake na kumrushia mawe, baada ya kukutana na Shenouda, huku wengine wakipambana na polisi waliokuwa wamesimama nje ya milango hiyo mikuu. Afisa wa polisi amesema kiasi askari polisi 40 wamepata majeraha madogo wakati waandamanaji hao walipowarushia mawe. Mapema waandamanaji hao walioandamana katika mji mkuu wa Cairo na Alexandria, walijaribu kumzingira kiongozi wa juu wa Waislamu na Imamu wa Al-Azhar, Ahmed al-Tayeb na kulibamiza gari lake.

Hata hivyo, siku moja baada ya kutokea shambulio hilo, Ibada ya Misa iliendelea jana katika Kanisa hilo la Coptic lililoko katika eneo la kaskazini mwa mji wa Alexandria. Hadi sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini kundi la Al-Qaeda limetaka adhabu ichukuliwe dhidi ya Wakristo wa madhehebu ya Coptic nchini Misri kutokana na tuhuma za kuwashikilia bila ridhaa yao, wake za mapadri wawili ambao walisema kwamba wamebadili dini na kuwa Waislamu.

Shambulio hilo limefanyika miezi miwili baada ya kundi lenye mafungamano na Al-Qaeda kudai kuhusika na shambulio la bomu katika Kanisa moja mjini Baghdad, Iraq na kuwaua watu kadhaa, wakisema lengo la shambulio hilo ni kushinikiza kuachiwa huru kwa mwanamke mmoja nchini Misri. Afisa wa polisi amesema kuwa watu 20 wanashikiliwa kwa ajili ya kuhojiwa, lakini hakukuwa na ushahidi wowote iwapo wanahusika moja kwa moja na shambulio hilo.

Rais Hosni Mubarak wa Misri ameahidi kupambana na ugaidi na kuushinda na kuwataka Wakristo na Waislamu wa Misri kuungana pamoja na kukabiliana na adui huyo.

Hata hivyo, magazeti ya serikali na yale binafsi jana yalionya kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaweza kutokea katika nchi hiyo. Shambulio hilo limelaaniwa vikali na viongozi mbalimbali wa kimataifa akiwemo kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita, ambaye aliwataka viongozi hao kuwalinda Wakristo dhidi ya mateso. Naye Rais Barack Obama wa Marekani aliliita shambulio hilo kama kitendo cha kikatili na kuchukiza. Wakati huo huo, akiwa katika Kanisa la mji wa kusini mwa Misri wa Aswan ambako alifanya ziara binafsi, Waziri Mkuu wa Ufaransa, Francois Fillon jana alisali kwa ajili ya kuwaombea waliouawa katika shambulio hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Josephat Charo

 • Tarehe 03.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zt3P
 • Tarehe 03.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zt3P

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com