1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya wasi wasi yatanda Tripoli

19 Mei 2014

Mji mkuu wa Libya umeendelea kuwa katika hali ya wasi wasi ikiwa ni siku moja baada ya vikosi vilivyo tiifu kwa generali muasi kulivamia bunge, kushambulia kambi ya anga na kutangaza kusitishwa kwa shughuli za bunge.

https://p.dw.com/p/1C2Nt
Jeshi la Libya katika shughuli za ulinzi mjini Tripoli.(18.05.2014)
Jeshi la Libya katika shughuli za ulinzi mjini Tripoli.(18.05.2014)Picha: picture-alliance/landov

Mji mkuu wa Libya umeendelea kuwa katika hali ya wasi wasi leo hii ikiwa ni siku moja baada ya vikosi vilivyo tiifu kwa generali muasi kulivamia bunge, kushambulia kambi ya anga na kutangaza kusitishwa kwa shughuli za bunge kwa kupinga uhalali wa serikali ya nchi hiyo ikiwa miaka mitatu baada ya kupinduliwa kwa dikteta Moummar Gaddafi.

Uongozi wa Libya umelani shambulio hilo la jana lililohanikiza ambapo watu wawili waliuwawa na wengine 50 kujeruhiwa na imeahidi kuendelea kuiongoza nchi hiyo.

Wanamgambo wakiwa na magari yenye mizinga ya kutungulia ndege na makombora walilivamia jengo la bunge katikati ya mji mkuu wa Tripoli na kupelekea wabunge kukimbia kuyanusuru maisha yao wakati wanamgambo hao wenye silaha wakizipekuwa ofisi za bunge hilo.

Masaa machache baadae kamanda mmoja katika kikosi cha polisi wa jeshini alisoma taarifa iliotangaza kusitishwa kwa bunge kwa niaba ya kundi linaloongozwa na Generali Khalifa Hifter aliewahi kuwa kamanda wa waasi ambaye alisema Marekani iliunga mkono juhudi zake za kumpinduwa Gaddafi katika miaka ya 1990.

Mokhtar Farnana akizungumza katika kituo kimoja cha televisheni nchini Libya kwa niaba ya kundi la Hifter amesema ameliagiza bunge la kuunda katiba lenye wajumbe 60 kusimamia shughuli za bunge. Farnana amesema bila ya kufafanuwa kwamba serikali ilioko sasa itafanya kazi kama baraza la mawaziri la dharura.

Kusitishwa kwa bunge

Farnana akiwa amevalia sare za kijeshi na kusimama mbele ya bendera ya Libya amesema wanaitangazia dunia kwamba hawawezi kuwa mahala pa mazalishio kwa ugaidi.

Generali Khalifa Haftar .(17.05.2014)
Generali Khalifa Haftar .(17.05.2014)Picha: Reuters

Ijumaa iliopita wanamgambo wanaomuunga mkono Generali Hifter waliyashambulia makundi mawili ya wanamgambo katika mji wa mashariki wa Benghazi ambapo wapiganaji 70 waliuwawa.

Serikali ya mpito ya Libya imelaani shambulio dhidi ya bunge katika taarifa iliotolewa usiku wa manane na kupuzilia mbali azimio lililotolewa na kundi la Generali Hifter.

Waziri wa sheria wa Libya Salah al-Marghani amesema katika taarifa kwamba serikali inalani kutowa maoni ya kisiasa kwa kutumia kikosi cha jeshi na kutowa wito wa kukomeshwa haraka kwa matumizi ya zana za kijeshi ambazo ni mali za wananchi na kuzitaka pande zote kutafuta usuluhishi kwa njia za mazungumzo.

Machafuko katika miji mikubwa miwili ya Libya yamezidi kuisogeza nchi hiyo kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuzusha wasi wasi nje ya nchi hiyo. Ubalozi wa Saudi Arabia leo umeufunga ubalozi wake na kuwahamisha wafanyakazi wake wa kibalozi kutoka nchi hiyo kwa kutumia ndege maalum.Mashirika mawili ya ndege ya Tunisia ya Tunisair na Syphax yamesitisha safari zake za ndege kwenda na kutoka Libya.

Bunge lagawika

Shambulio dhidi ya bunge hapo jana mjini Tripoli limewalenga wabunge na maafisa wa serikali ambao Hifter anawalaumu kwa kuwaachilia watu wenye itikadi kali za Kiislamu kuishikilia mateka nchi hiyo.

Bunge la Libya katika kikao.
Bunge la Libya katika kikao.Picha: Mahmud Turkia/AFP/Getty Images

Bunge la Libya limegawika kati ya makundi ya itikadi kali za Kiislamu na yale yanayopinga itikadi kali yakiungwa mkono na wanamgambo wanaopingana.

Hivi karibuni Waislamu wa itikadi kali waliunga mkono kuchaguliwa kwa waziri mkuu mpya aliyesusiwa na wale wenye kupinga itikadi kali za Kiislamu ambao wamesema serikali mpya itakuwa sio halali.

Haiko wazi wanamgambo na wanasiasa gani wanamuunga mkono Hifter lakini shutuma zake zinaungana na hali ya kutoridhika kwa jumla ilioko miongoni mwa wananchi kwa jumla kwa serikali yao isiokuwa na nguvu kabisa.

Umoja wa Ulaya umesema una wasi wasi mkubwa kwa ghasia zinazotokea Libya. Tayari bei za mafuta zimepanda kutokana na wasi wasi wa kutibuka kwa uzalishaji wa mafuta kutoka nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman