1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin Terrorverdächtige Festnahme

9 Septemba 2011

Ujerumani imeongeza hali ya tahadhari tangu baada ya shambulio la kigaidi nchini Marekani. Sheria kadha zimebadilika licha ya kuwa hakuna sababu ya kutaharuki.

https://p.dw.com/p/12WIp
Picha ya eneo lililoshambuliwa mjini New York la Ground Zero.Picha: AP

Ujerumani tangu baada ya shambulio la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001 dhidi ya Marekani, imeongeza hali ya tahadhari. Sheria kadha zimebadilishwa, kituo kipya cha kupambana na ugaidi kilianzishwa kwa mfano wa Marekani, mashirika ya ujasusi yakaimarishwa. Makundi ya Waislamu ambao wako tayari kufanya hujuma wanaofikia kiasi ya 100 hadi 200, ambao wamekuwa wakichunguzwa na wataalamu, wamekuwa wakiendelea kuchunguzwa wakati wote na idara ya uhalifu ya Ujerumani. Kitisho kipo na kinaendelea, lakini kutokana na kile tunachofahamu hakuna sababu ya kubweteka.

Hali hiyo, haijabadilika hata baada ya kukamatwa hivi karibuni kwa watuhumiwa mjini Berlin. Ishara kamili kuhusu shambulio hasa bado haijapatikana. Hadi hivi karibuni ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali haikuwahi kufanya uchunguzi.

Hali ya usalama nchini Ujerumani haijabadilika. Jaribio la kununua kiasi kikubwa cha kemikali, imesababisha wananchi kutoa taarifa ambazo zimewezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao wawili.

Hilo peke yake linatoa ishara kuwa wengi wa Wajerumani wanatambua hatari jumla iliyopo na wanaonyesha kutoridhishwa kwao na mashambulio yanayoongezeka ya kigaidi.

Miaka kumi iliyopita hali isingekuwa hivyo. Kwa upande mwingine hakuna sehemu ya Ujerumani ambayo inaonekana kuwa na wasiwasi mkubwa wa ugaidi. Inawezekana pia ni kutokana na maafisa mwaka jana, walipotoa tahadhari ya kuchukuliwa hatua za usalama kutokana na uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi lakini kwa bahati nzuri, hakuna kilichotokea.

Pia katika wakati huu mtu anapokumbuka matokeo ya kusikitisha ya shambulio la Septemba 11, Wajerumani wengi hawataki kuishi katika taifa linalodhibitiwa kipolisi. Hatari ya ugaidi ni kitu cha kweli, inawezekana popote pale duniani ikatokea. Lakini hakuna sababu, kuishi katika hofu daima ama kuachana na uhuru tulionao wa kiraia. Hifadhi ya takwimu inaweza kufanyika tu kwa misingi ya hatua maalumu za usalama. Uhuru wa mtu binafsi ni lazima uendelee kulindwa. Hii ni pamoja na mamilioni ya Waislamu, ambao ni raia wa Ujerumani na pia wale ambao si raia wa Ujerumani lakini wanaishi nchini Ujerumani. Ujerumani katika miaka iliyopita imeweza kupata mchanganyiko baina ya kupandisha kiwango cha tahadhari na hali ya kawaida ya kuishi bila hofu.

Mwandishi : Daniel Scheschkewitz / ZR / Sekione Kitojo.

Mhariri : Josephat Charo