1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Hali Syria na kudhalilishwa wanawake

Oumilkheir Hamidou
27 Septemba 2016

Hali nchini Syria ambapo vita vinaendelea na watu wanauawa kila siku pamoja na mjadala kuhusu visa vinavyowadhalilisha wanawake ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2QdL6
Syrien Aleppo Trümmer nach einem Luftangriff
Picha: Reuters/A.Ismail

Tuanzie lakini Syria ambako mabomu yanaendelea kufyetuliwa na maisha ya binaadam yanazidi kuangamia.Walimwengu wanafanya nini? Linajiuliza gazeti la mjini Fulda-"Fuldaer Zeitung" na kuendelea kuandika:"Picha za televisheni ukiziona zinakusisimua mwili na kuhuzunisha: raia wasiokuwa na idadi wanapigwa mabomu na maguruneti na kuteketezwa. Muimla Assad na mshirika wake mkubwa wameingia katika awamu ya mwisho ya kuuhujumu mji huo. Na yote hayo yanatokea na ulimwengu ukishuhudia. Anaetaka anaweza kufuatilizia mauwaji hayo kupitia mtandao. Na walimwengu je wanafanya nini? Wanafumba macho. Hali hiyo inahuzunisha na kusikitisha. Mengi yanadhihirisha kwamba Aleppo utaingia katika madaftari ya historia kama tukio jengine lililoiaibisha jumuia ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa,baada ya Srebrenica na Rwanda.

Waimla wanatandika na kupuliza

Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linamulika mchango wa Urusi katika janga la Syria. Gazeti linaendelea kuandika:"Putin anatunisha misuli bila ya kujali,lengo ni kujionyesha na kueneza hofu na vitisho. Si mageni kwa yeyote yule kwamba tangu enzi za enzi,waimla wakitaka kujiimarisha madarakani hawachelei kutumia viboko: Kauli mbiu: Kuendelea kung'ang'ania madaraka kupitia matumizi ya nguvu na vitisho.

Wanawake wanaendelea kudhalilishwa

Mada ya pili magazetini hii leo inahusu mjadala  uliozushwa na mbunge mmoja wa chama cha Christian Democratic Union CDU,anaelalamika dhidi ya madhila anayokumbana nayo kwasababu yeye ni mwanamke. Gazeti la "Mitteldeutsche " la mjini Halle linasema madhila kama hayo ya kijinsia yana madhara sawa na yale ya kuingiliwa kwa nguvu kimwili. Gazeti linaendelea kuandika:"Suala hapa halihusu pekee mwanamke kudhalilishwa kingono. Linakwenda mbali zaidi na kuandaliwa kwa werevu mkubwa zaidi;ni suala la kumvunjia hadhi na kumbagua kivitendo na kwa maneno, mwanamke. Mpaka kati ya upotofu na dhana,kati ya upumbavu na madhila,unatofautiana sana lakini hiyo isimaanishe kwamba kila kitu kinaruhusiwa. La muhimu zaidi ni kuheshimiana. Kwa bahati mjadala umezushwa hivi sasa na ujumbe uliokuwa umeenea katika mtandao wa kijamii Tweeter umeshafutwa. Anaetaka kuupata lakini analazimika kutumia kifungo ziada.

Tatizo la kudhalilishwa kijinsia hata kupitia maneno halikuanza leo,linaandika gazeti la "Stuttgarter Nachrichten"linalokumbusha kisa kama hicho kilichowahi kumsibu mwandishi habari wa jarida la Stern kutoka kwa mwanasiasa wa chama cha kiliberali,Rainer Brüderle miaka mitatu. Gazeti linaendelea kuandika:"Katika hali kama hii,kuna njia mbili za kujibu. Mtu anaweza kama ilivyotokea miaka mitatu iliyopita katika kadhia ya Brüderle kuacha muda upite,kushuku kilichosemwa na mdhalilishwa na pengine kufika hadi ya kutoamini alichokisema. Kimsingi kuna sababu ya hali kama hiyo. Kwasababu kuna masuala mengi yanayochomoza na ambayo hayajapatiwa majibu. Ni ukweli wa mambo kwamba baadhi ya dhana mtu hawezi kuzitolea ushahidi au kubisha. Njia nyengine ni kutomtanguliza mbele mwanamke,badala yake kile kisa chenyewe hasa. Upotofu kama huo wa kingono sio tu ni jambo la tangu zamani bali bado lingalipo tena kila mahala.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Yusuf Saumu