1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ni shwari mpakani mwa Kongo na Uganda

7 Julai 2012

Hali katika eneo la mpaka kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeripotiwa kuwa ya utulivu Jumamosi (07.07.2012) baada ya mapambano kati ya kundi la waasi na majeshi ya Kongo

https://p.dw.com/p/15TPS
Vikosi vya serikali ya Kongo vikiwa katika mji wa Bunagana ambao sasa umetekwa na waasi.
Vikosi vya serikali ya Kongo vikiwa katika mji wa Bunagana ambao sasa umetekwa na waasi.Picha: dapd

Kundi la waasi la M23, linaloongozwa na generali alieasi Bosco Ntaganda ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC kwa kuhusika na uhalifu wa kivita limeimarisha udhibiti wake kwa mji wa mpakani wa Bunagana lakini kumekuwa hakuna mapigano kwa zaidi ya saa 24.Mwanajeshi mmoja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India aliuwawa hapo awali.

Msemaji wa kijeshi wa Uganda Kapteni Peter Mugisha ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba " Waasi wanaudhibiti mji wa Bunagana lakini hali ni shwari.Kumekuwa hakuna mapigano tokea Ijumaa asubuhi.Tumeimarisha uchunguzi wa usalama mpakani na kuwakaguwa wakimbizi wote.

Mwanajeshi wa serikali ya Kongo akiwa katika doria mashariki mwa nchi hiyo.
Mwanajeshi wa serikali ya Kongo akiwa katika doria mashariki mwa nchi hiyo.Picha: Reuters

Wanajeshi 600 wa Kongo wakimbilia Uganda

Zaidi ya wanajeshi 600 wa serikali ya Kongo waliikimbia medani ya mapambano hapo Alhamisi na kutafuta hifadhi nchini Uganda baada ya kuzidiwa nguvu na waasi wa kundi la M23.Hapo Ijumaa mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India aliuwawa katika mapambano.

Kwa mujibu wa Mugisha wakimbizi bado wanaendelea kukimbilia Uganda ingawa sio kwa idadi kubwa.Amesema hakuna wanajeshi wengine waliokimbilia nchini humo ziada ya wale 600 waliokimbilia Uganda hapo Alhamisi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR na mashirika mengine yamekuwa yakiwaorodhesha wakimbizi.

Mapigano yamepamba moto hivi karibuni kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 ambao ni waasi wa zamani waliojumuishwa kwenye jeshi la taifa hapo mwaka 2009 na kuasi tena baadae.Taifa hilo la Afrika ya kati ukubwa wake ni sawa na theluthi mbili ya ukubwa Ulaya ya magharibi.

Chama cha Msalaba Mwekundu cha Uganda kimesema hapo Ijumaa maelfu ya watu wamekuwa wakikimbilia nchini humo siku mbili zilizopita kukimbia umwagaji damu na kwamba wamejiunga na maelfu ya wakimbizi wenzao wa Kongo ambao tayari wako Uganda.

Wanajeshi wa Kongo wakijiandaa kwa mapambano mashariki mwa Kongo.
Wanajeshi wa Kongo wakijiandaa kwa mapambano mashariki mwa Kongo.Picha: Reuters

Rwanda yalaumiwa kwa kuwasaidia waasi wa Kongo

Repoti ya kufadhaisha ya Umoja wa Mataifa iliotolewa mwezi uliopita imeituhumu Rwanda kwa kuwapatia silaha waasi wa kundi la M23 ambao wana mafungamano na wanamgambo wa Kitutsi.

Serikali ambayo kwa kiasi kikubwa inadhibitiwa na Watutsi huko Kigali imekanusha vikali madai hayo na kutowa wito wa kukomeshwa kwa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambapo ni mahala penye kikosi kikubwa kabisa cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa duniani wanaofikia wanajeshi 2,000.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo taifa kubwa lenye utajiri wa madini lakini lililokumbwa na umaskini likiwa na watu milioni 71 lilimaliza vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe hapo mwaka 2003 juu ya kwamba wanamgambo bado wanaendelea na harakati zao katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ambapo kumekuwapo na mizozo ya kila mara.

Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni 5 wamekufa kwa sababu ya vita hivyo nchini Kongo tokea miaka ya 1990 ambapo wengi wao wamekufa kutokana na maradhi .

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa

Mhariri: Abdulrahman ,Mohamed