1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ngumu ya maisha Malawi

Mohammed Abdul-Rahman22 Februari 2007

Wengi wanalazimika hata kuuza baadhi ya vyombo vyao vya majumbani ili kupata fedha kuwalipia watoto wao, ada za shule.

https://p.dw.com/p/CHla
Mmoja kati ya miradi michache ya maji safi nchini Malawi
Mmoja kati ya miradi michache ya maji safi nchini MalawiPicha: Zimmermann

Grace Kafere ni mama wa miaka 54 mwenye watoto watano, akiishi bila ya mume. Alipoteza kazi yake kama karani msaidizi miaka mitatu iliopita baada ya mageuzi katika kampuni aliyokua akifanya kazi, na tangu wakati huo ameshindwa kupata kazi nyengine.

Ili aweze kupata fedha za kuwalipia ada ya shule wanawe,, hulazimika mpaka kuuza vyombo vya nyumbani kama jiko la umeme. Mwanawe mkubwa ana umri wa miaka 16 na yuko shule ya sekondari.

Mama huyu anasema ameuza kila kilicho na thamani na sasa anajaribu kufanya biashara ndogo ili watoto waweze kuendelea na shule. “Ninauza kila kitu anasema Bi Kafere, chochote ninachoweza kukusanya mpaka kuni ambazo huwauzia majirani anasisitiza.”

Kwa upande mwengine, anashindwa kumudu kununua kila siku mahitaji muhimu ya chakula kama mkate na sukari na familia ina kula mara moja tu kwa siku, badala ya mara tatu kama ilivyokua desturi hapo zamani.

Aidha wamelazimika pia kuhama katika nyumba ya vyumba vitatu katika eneo moja la maisha ya wastani na kuhamia katika nyumba ya chumba kimoja cha kulala katika eneo moja la wakaazi masikini katika kitongoji cha Blantyre. Hulala pamoja na mabinti zake watatu na mwanawe wa kiume akilala ukumbini.

Mkaazi mwengine kwa jina Jackson malire anaungama kwamba maisha ni magumu mno. Akiwa na familia ya watu 6, wote hutegemea pato la kazi yake kama mlinzi wa usiku akilipwa dola 20 za kimarekani kwa mwezi.

Wamalawi wengi wanatapia maisha katika hali sawa na hizo.

Baina ya 2005 na 2006 Malawi ilianguka kutoka nafasi ya 10 hadi ya 11 katika orodha ya dunia ya nchi 30 masikini kabisa ulimwenguni. Katika ripoti ya utafiti ya Shirika la mpango wa maendeleo la umoja wa mataifa iko nafasi ya 166 miongoni mwa nchi 177.

Zaidi ya 65 asili mia ya Wamalawi milioni 12 wanaishi chini ya kiwango cha umasikini cha dola moja ya kimarekani kwa siku.

Matatizo mengine ni vifo miongoni mwa watoto wanaozaliwa ikiripotiwa hufariki zaidi ya watoto 1,100 kwa kila laki moja wanaozaliwa.

Theluthi moja ya wamalawi hawana maji safi na matokeo ni magonjwa au kifo kutokana na kuharisha na kipindu pindu. Ukimwi ni changa moto nyengine kubwa inayoikabili Malawi,ikikadiriwa mmoja katika kila watu 10 ameathirika.

Kwa jumla sambamba na hali ngumu ya maisha. Umri wa wastani wa kuishi ni miaka 39 kiwango cha chini kabisa duniani. Na wadadisi matatizo hayo katika maisha ya sehemu kubwa ya umma wa Malawi yanaathiri mafanikio yake katika kufikia lengo la kwanza la maendeleo ya milenia la umoja wa mataifa.