1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Syria

4 Septemba 2012

Kiongozi mpya wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, Peter Maurer, amezungumza na rais Bashar al Assad kwa lengo la kurahisisha njia za kupatiwa misaada ya kiutu wasyria wanaosumbuliwa na mapigano.

https://p.dw.com/p/1639O
Nembo za shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilal NyekunduPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, Hicham Hassan, mazungumzo kati ya Peter Maurer na rais Bashar al Assad yalidumu dakika 45.

Kutokana na shida za kufikia maridhiano ya jinsi ya kuufumbua mzozo unaoendelea nchini Syria, jumuia ya kimataifa inalenga zaidi juhudi zake katika kuwapatia misaada ya kiutu watu milioni moja na laki mbili walioyapa kisogo maskani yao kwasababu ya vita, na kulazimika kuishi katika majengo ya serikali, pamoja pia na wakimbizi laki mbili na 21 elfu waliomiminika katika nchi jirani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, jumla ya watu milioni mbili na nusu wanaathirika na vita na idadi ya wanaoyapa kisogo mapigano inazidi kuongezeka.

Kwa mujibu wa shirika la haki za binaadam la Syria, lenye makao yake makuu mjini London, mapigano hayo yamezidi makali mnamo wiki za hivi karibuni: watu 5000 wameuwawa mwezi uliopita.

Syrien Flüchtlinge Grenze Türkei
Wakimbizi wa Syria katika eneo la mpakani na UturukiPicha: picture-alliance/dpa

Mkuu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, Peter Maurer, aliyewasili Damascus jana usiku, ataendelea na ziara yake nchini Syria hadi alkhamisi ijayo, ambapo atazungumza pia na waziri wa mambo ya nchi za nje, Walid Mouallem; waziri wa mambo ya ndani, Mohammed al Shaar; na waziri wa afya, Saad Abdelsalam Nayef. Hakupanga lakini kuonana na wawakilishi wa upande wa upinzani.

Mkuu wa baraza la taifa la Syria linaloyaleta pamoja makundi tofauti ya upande wa upinzani, Abdel Basset Sayda, ametoa mwito kwa mara nyengine tena wapatiwe silaha na kuihimiza jumuia ya kimataifa iingilie kijeshi ili kama anavyosema "kuwalinda raia".

Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, anasema:

"Tunahitaji msimamo bayana na thabiti wa jumuia ya kimataifa kwa lengo la kukidhi matakwa ya umma wa Syria.Tunahitaji ufumbuzi wa kisiasa."

Syrien bewaffnete Rebellen
Waasi wa SyriaPicha: AP

Mapigano bado yanaendelea; watu 150, wengi wao ni raia wa kawaida, wameuwawa kufuatia mapigano ya jana kote nchini Syria.

China imesema kwa mara nyengine tena hii leo inapinga uamuzi wowote wa kuingilia kijeshi nchini Syria.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje, Hong Lei, amekiri mjini Beijing kwamba hali inazidi kuwa mbaya nchini Syria. Hata hivyo, anashadidia umuhimu wa kuimarishwa umoja nchini humo.

Mwandishi:AFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman