1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali Cote d'Ivoire yaendelea kuwa tete

27 Desemba 2010

Nchini Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara, alietajwa na kamati ya uchaguzi kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Novemba 28, ametoa wito wa mgomo nchini kote kuanzia leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/zqDq
Vikosi vya UN vikifanya doria mjini AbidjanPicha: AP

 Bwana Alassane Ouattara amewataka raia kususia kazi, hadi Laurent Gbagbo atakapokubali kuondoka madarakani.

Msemaji wa Alassane Ouattara, Bwana Patric Achi, amesema kwamba uamuzi wa kuitisha mgomo wa kitaifa, ni hatua nyingine inayolenga kumlazimisha Bwana Laurent Gbagbo kuondoka madarakani.

Lakini upande wa Gbagbo haujachelewa kujibu madai ya mpinzani wake, kwa kuonya kuwa hali hiyo itazidi kuihatarisha hali ya kiuchumi na usalama, ambayo tayari ni mbaya mno.

Habari kutoka Abidjan mji mkuu wa Cote d'Ivoire zinasema, kwamba baadhi ya wafanyakazi wa serikali ambao tangu mwezi mzima sasa tayari walikuwa wachache kwenda kazini, leo wamesalia nyumbani. Baadhi ya wafanyabiashara pia hawakufungua maduka.

Wakati huo huo, wanasubiriwa kuwasili mjini Abidjan, marais watatu wa nchi za Jumuiya ya Uchumi wa mataifa ya Afrika ya magharibi ECOWAS, kesho Jumanne.

Marais wa Benin, Cape Werde na Sierra Leonne, wanatazamiwa kumpelekea Bwana Laurent Gbagbo ujumbe, ambao inasemekana kuwa ni wa mwisho kabla ya kuchukuliwa hatua kali, kumtaka aondoke madarani haraka iwezekanavyo.

Lakini hata kabla ya marais hao kuwasili mjini Abidjan, Katibu mkuu wa Jumuiya hiyo, Victor James Ogbeho, amesema kwamba ikiwa Bwana Gbagbo atataka kung'ang'ania madarakani, basi jumuiya itakuwa haina njia nyingine, ila tu kutumia nguvu.

" Ikiwa Bwana Gbagbo atashindwa kutimiza maombi ya ECOWAS, jumuia itakua haina njia nyingine, ila tu kuchukua hatua nyingine, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu; ili kufikia matakwa ya raia wa Cote d'Ivoire".

Huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kumchukulia hatua Laurent Gbagbo ili kumshinikiza kuondoka madarakani,katika mazungumzo hapo jana na gazeti la Ufaransa le Figaro, yeye amesema kwamba ataendelea kutetea kile alichokielezea kuwa ushindi wake dhidi ya njama ya jamii ya kimataifa, kutaka kumuweka madarakani mpinzani wake Alassane Ouattara.

Ameishtumu Ufaransa na Marekani kuwa ndizo zinazoongoza njama hizo, akisema yuko tayari kuwapokea marais wanaotarajiwa kuwasili kesho mjini Abidjan kama ndugu na marafiki.

Bwana Laurent Gbagbo ambaye amewekewa vikwazo vya kusafiri Ulaya na Marekani, jana ndege yake ilizuiliwa na serikali ya Ufaransa kwenye uwanja wa ndege wa Mulhouse nchini humo, ambapo ilikuwa ikifanyiwa uchunguzi.

Laurent Gbagbo amesema kwamba ikiwa jumuiya ya ECOWAS itaamua kuanzisha harakati za kijeshi dhidi yake, basi itakuwa ni mara ya kwanza ambapo viongozi wa kiafrika wanatumia nguvu kwa pamoja, kumuondoa madarakani kiongozi mwingine wa kiafrika.

Akaonya hatua hiyo inaweza kusababisha maafa makubwa, siyo tu kwa Cote d'Ivoire, lakini pia katika eneo zima, hasa kwa kuwa nchini Cote d'Ivoire wanaishi raia wengi kutoka nchi jirani.

Mwandishi: Jean-Francois Gisimba /AFP

Mhariri: Josephat Charo