1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado ni tete nchini Myanmar

Abou Liongo27 Septemba 2007

Mtu mmoja ameuawa na wengine zaidi ya watano wamejeruhiwa baada ya majeshi ya usalama ya Myanmar kufyatua risasi katika juhudi za kuzima maandamano ya amani kuipinga serikali ya kijeshi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/CB0w
waandamanaji wakisambaratishwa na polisi mjini Rangoon
waandamanaji wakisambaratishwa na polisi mjini RangoonPicha: AP

Aidha mamia kadhaa ya waandamanaji wakiwemo watawa wa kibuddha wamekamatwa katika harakati hizo.

Mashuhuda wanasema kuwa idadi kubwa ya watawa hao wa kibuddha ambao wanaheshimika nchini humo walipigwa na kubururwa kwenye magari ya jeshi.Hiyo ni baada ya wananchi hao waliungana na watawa katika maandamano kukaidi amri ya kuwataka kubakia majumbani mwao.

Mjini New York Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura kuzungumzia hali hiyo huko Mynmar ambayo zamani ikiitwa Burma.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alitoa wito kwa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo kufanya kila linalowezekana kuzuia maandamano hayo kwa njia ya amani.

Amesema kuwa anatarajia kuelekea Myanmar kusaidia kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa kwa njia ya majadiliano.

Wakati huo huo China imesema kuwa kuiwekea vikwazo Myanmar hakutasaidia kitu.

Baadhi ya wanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanaona suala la Myanmar ni la kimataifa, lakini Urusi na China zinasema ni suala la ndani ya nchi.

Mjini London, Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwa na sauti moja dhidi ya utawala huo wa Myanmar.