1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shauku ya mabadiliko Ujerumani ni ndogo kabla uchaguzi

Josephat Charo
24 Agosti 2017

Mwezi mmoja kabla uchaguzi mkuu Ujerumani Septemba 24, shauku ya mabadiliko ni ndogo. Mgombea wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, Angela Merkel anaonekana kuelekea kupata ushindi kwa muhula wa nne kama kansela.

https://p.dw.com/p/2ikMC
Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Ostrop

Merkel au Merkel - Je hilo ndilo chaguo la Ujerumani? ndilo swali kuu lililoulizwa na kipindi cha televisheni kinachorushwa kila Jumapili, huku matokeo ya kura za maoni yakionesha muungano wa kihafidhina wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union, CDU, na Christian Social Union, CSU, ukizidi kuongoza na kutanua pengo kati yake na mahasimu wao wa chama cha Social Democratic, SPD.

Baada ya miaka 12 ya Merkel au "Mutti", Ujerumani haina shauku ya kutaka mabadiliko, ndivyo lilivyoandika katika makala yake gazeti linalochapishwa kila siku Ujerumani, Die Welt.

Akitajwa mara kwa mara kama mwanamke mwenye ushawishi mkubwa kabisa ulimwenguni, Merkel, mwenye umri wa miaka 63, amejitokeza katika mikutano ya kampeni akitetea ujasiri wake, akituma ujumbe wa uthabiti na muendelezo katika ulimwengu unaokabiliwa na hali ya kuyumba kutokana na mchakato wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya, Brexit, na Donald Trump kushinda urais wa Marekani.

Akizungumza mbele ya wafuasi takriban 5,000 wa chama chake cha CDU Jumanne wiki hii mjini Münster, Merkel alitetea uamuzi wa chama kudhibiti deni la taifa.

"Tulichopanga ni kwamba tutaendelea kufanikiwa katika yale ambayo tayari tumeyaonesha miaka minn eiliyopita: Hakutakuwa na madeni mapya katika ngazi ya ya shirikisho."

Bremen Marin Schulz Beginn Wahlkampftour
Picha: picture-alliance/dpa/M. Bahlo

Hotuba nyingi za Merkel zimejikita zaidi katika ukuaji uchumi na kupungua kwa kiwango kikubwa ukosefu wa ajira Ujerumani. Kama chama chake cha CDU, vyama vingi havijalipa kipaumbele suala la uhamiaji katika kampeni zao.

Schulz amkosoa Merkel

Juhudi za Merkel zimetofautiana kwa kiwango kikubwa na za mpinzani wake mkuu, mgombea ukansela wa chama cha SPD, Martin Schulz, ambaye amekuwa akizuru maeneo mbalimbali ya Ujerumani akiahidi kutetea taifa lenye haki zaidi.  Schulz amemkosoa Merkel kwa kuminya demokrasia kwa kushindwa kuweka bayana mpango wake kwa miaka minne ijayo.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni jana mjini Goettingen, Shulz alisema, kinyume na Merkel, atapinga masharti ya rais Trump kuzitaka nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO kuongeza matumizi yao katika masuala ya ulinzi.

Schulz aidha alisema Ujerumani haitakiwiki katika mazingira yoyote yale kushiriki mikakati ya kujihami kwa silaha za nyuklia. "Ni wazi kutokana na sera za rais wa Marekani Donald Trump kwamba jambo hili ni sehemu ya mpango wake. Tumeshuhudia katika mzozo wa Korea Kaskazini kwamba tunahitaji mikakati ya kuangamiza silaha za nyuklia badala ya kujihami, akaendelea kusema Schulz. Ndio maana ninataka silaha za nyuklia zilizowekwa nchini Ujerumani ziondolewe."

Vyama vingine vinne vidogo vinatarajiwa kupata asilimia tano ya kura kuweza kuwakilishwa katika bunge la Ujerumani, Bundestag, jambo ambalo halijawahi kutokea.

Chama kinachopendelea biashara, FDP, ambacho kina matuamini ya kufanya vyema baada ya kushindwa vibaya na kukosa uwakilishi bungeni mwaka 2013, pamoja na chama cha Kijani, vinatajwa kuwa na fursa ya kuwa washirika katika serikali ya kihafidhina ya kansela Merkel.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef