1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna mpasuko wa uhusiano kati yetu;Obama, Netanyahu

7 Julai 2010

Bw Netanyahu asema yuko tayari kukutana na Mahmoud Abbas wa Palestina kwa mazungumzo.

https://p.dw.com/p/OCho
Rais Barack Obama na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika ikulu ya Marekani.Picha: AP

Rais wa Marekani, Barack Obama amesema anatarajia mazungumzo ya ana kwa ana mashariki ya kati kuanza kabla ya mwisho wa mwezi Septemba, huku kiongozi huyo na waziri wa Israel, Benjamin Netanyahu wakikanusha madai kwamba kuna mpasuko katika uhusiano wao.

Viongozi hao waliketi karibu na walisalimiana kwa muda mbele za kamera wakinuia kusitisha wasiwasi uliojiri katika mkutano wao wa faragha wa mwezi machi katika ikulu ya Marekani

Rais wa Marekani, Barack Obama amesema anaamini kwamba waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anataka amani na kwamba anaamini yuko tayari kuchukua hatua mahsusi kwa ajili ya amani. Rais Obama aliyasema hayo huku akilipinga suala lililoashiria kwamba alikuwa ameitenganisha Marekani kutoka kwa Israel.

Bw Obama alisema kilicho wazi ni kwamba amekuwa akimuamini waziri mkuu Netanyahu tangu akutane naye kabla ya kuchaguliwa raia na kwamba amekiri hivyo hadharani na faraghani.

Mazungumzo hayo yalifanyika wakati kukiwa hali ya wasiwasi kuhusiana na na kusitishwa kwa muda, ujenzi wa makaazi kwa walowezi wa kiyahudi na muda huo unakamilika mwishoni mwa mwezi Septemba.

Rais Obama akiligusia suala hilo alisema anatarajia mchakato wa mazungumzo ya ana kwa ana kutoka kwa ule wa upatanishi unaoongozwa na Marekani kati ya Wa-Israeli na Wapalestina, yataufanya muda huo wa mwisho usiwe na maana.

Bw Netanyahu amesema yuko tayari kukutana na kiongozi wa mamlaka ya ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas wakati wowote lakini Wapalestina bado hawajajitolea kwa mazungumzo ya ana kwa ana huku wakiituhumu Israel kwa kudharau mazingira hayo kwa kuendeleza juhudi za ujenzi wa makaazi. Bw Netanyahu alisema walijadiliana kuhusu mkakati muafaka utakaofuatwa sasa.

Changamoto kwa sasa ni kuwashawishi Wapalestina kukubali muda wa utekelezaji ambao rais Barack Obama anao akilini. Kulingana na Nabil Abu Rudeina, msemaji wa Rais wa Mamlaka ya ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas, kionmgozi huyo anasisitiza juu ya umuhimu wa mazungumzo ya upatanishi kuhusu masuala tete ya mipaka na usalama, kabla ya kuingia katika mazungumzo ya ana kwa ana.

Waziri mkuu wa Israel anashinikizwa na chama chake cha mrengo wa kulia kwamba asiyafuate matakwa ya Marekani ya kusogeza mbele muda wa kusitisha ujenzi.

Bw Netanyahu anakutana leo na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa , Ban Ki moon na ameonya kwamba kitisho kwa Israel ni mpango wa nyuklia wa Iran na aliupigia upatu juhudi ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Iran.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohamed