Hakuna dalili ya makubaliano kati ya Iran na IAEA | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hakuna dalili ya makubaliano kati ya Iran na IAEA

Mazungumzo baina ya Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki IAEA Yukia Amano na Viongozi wa Iran, kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo hayajaonyesha dalili ya kufikia makubaliano.

Mkuu wa IAEA Yukiya Amano akiwa mjini Tehran Iran

Mkuu wa IAEA Yukiya Amano akiwa mjini Tehran Iran

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki IAEA Yukia Amano, amefanya mazungumzo na Iran juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo ambao umegubikwa na utata. Mazungumzo hayo hayajaonyesha dalili yoyote ya kufikia makubaliano hadi sasa.

Amano amefanya ziara Iran baada ya nchi hiyo kuonyesha dalili ya za kukubali ukaguzi wa IAEA kwenye mradi wake wa kurutubisha madini ya Uranium ambao mataifa ya magharibi yanaushuku kuwa ni maandalizi ya kutengeneza silaha za atomiki.

Hadi sasa Amano amekwishazungumza na Mkuu wa Taasisi ya Nyuklia ya Iran Fereydoun Abbas Davan pamoja na Kiongozi wa mazungumzo ya nyuklia wa nchi hiyo Saeed Jalili atakayeshiriki mkutano wa Baghdad baina nchi yake na Mataifa Yenye Nguvu Duniani hapo kesho.

Pamoja na kukosekana kwa dalili za makubaliano, Amano ana matumaini makubwa kutokana na Iran kuonyesha ushirikiano mzuri baina yake na IAEA.

Kiongozi huyo amesema kuwa mazungumzo baina yake na viongozi hao wa Iran yamefanyika katika mazingira mazuri na kwamba anaamani yatafungua njia ya kufikia muafaka kwenye mkutano wa Baghadad.

Marekani yatangaza vikwazo dhidi ya Iran

Katikati ya matumaini hayo ya Amano, vinaibuka vikwazo kutoka kwa Marekani vikiadhimia kuikwamisha Iran kiuchumi kama hatua mojawapo ya kuishinikiza kukubali ukaguzi wa miradi yake ya nyuklia.

Barack Obama, Rais wa Marekani

Barack Obama, Rais wa Marekani

Baraza la wawakilishi la Marekani limepitisha muswada wa sheria wa Desemba mwaka jana na sasa ni lazima limalize tofauti zake na Baraza la Seneti kuhusu suala hilo.

Vikwazo hivyo vimeyalenga mapato ya mafuta ya Iran kwa kusitisha mikataba ya kiuchumi na mataifa ambayo ni wateja wakubwa wa nchi hiyo pamoja na makampuni makubwa ya kuhifadhia nishati hiyo.

Nchi za magharibi pamoja na Israel zinaamini kuwa urutubishaji wa madini ya Uranium unaofanywa na Iran ni maandalizi ya kutengeneza silaha za nyuklia, lakini Iran yenyewe imekana shutuma hizo ikisema mpango huo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni pamoja na kujipatia umeme na matibabu ya saratani.

Seneta wa Chama cha Demokrat Robert Menendez aliyekuwa mstari wa mbele kwenye uandikaji wa muswada huo, amesema kuwa kupitishwa kwake kabla ya mkutano wa Baghdad ni alama ya kuiambia Iran kuwa Marekani haina mchezo na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo na kwamba kitendo cha kupoteza muda kwenye mazungumzo hakitaisaidia.

Vikwazo hivyo vipya ambavyo vilipitishwa chini ya sheria na kutiwa saini na Rais wa Marekani Barack Obama, vinahusu pia utozaji wa faini kwa makampuni yatakayofanya bishara na Benki Kuu ya Iran.

Iran ambayo ni msafirishaji wa tatu wa mafuta duniani itazungumza na mataifa ya China, Marekani, Uingereza, Urusi, Ufaransa pamoja na Ujerumani.

Mkuu wa IAEA Yukiya Amano akiwa mjini Tehran, Iran

Mkuu wa IAEA Yukiya Amano akiwa mjini Tehran, Iran

Israel nayo imepaza sauti kuyataka mataifa hayo kutokuwa na msalie na Iran kwenye mazungumzo, ikiamini kuwa nchi hiyo iko mbioni kutengeneza silaha za atomiki kwa lengo la kuingamiza. Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa ni lazima mataifa hayo yaonyeshe uimara na si udhaifu kwenye mazungumzo hayo.

Mwandishi: Stumai George/APE/REUTRS/DPAE

Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com