1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakimu aamuru kuachiliwa huru kwa wafungwa sita wa Guantanamo

Mohamed Dahman21 Novemba 2008

Zaidi ya miaka saba baada ya kufunguliwa kwa gereza la Guantanamo hakimu wa Marekani kwa mara ya kwanza leo amekiri kwamba baadhi ya mahabusu walikuwa wanashikiliwa kinyume na sheria na kuamuru kuachilwa kwao huru.

https://p.dw.com/p/FzRp
Gereza la Guantanamo.Picha: AP

Na katika pigo jengine kwa utawala wa Rais George W. Bush wa Marekani hakimu huyo ameamuru kwamba wafungwa watano Waalgeria waliokamatwa hapo mwaka 2001 waachiliwe huru kutoka gereza hilo la kijeshi lilioko kusini mwa Cuba lililojengwa kushikilia watuhumiwa wa ugaidi.

Hakimu Richard Leon amesema mahkama serikali imeshindwa kuonyesha kwa uzito wa ushahidi kwamba watuhumiwa hao watano walikuwa wamepanga kwenda nchini Afghnanistan kushiriki katika mapambano dhidi ya vikosi vya Marekani.

Lakini Leon ameona kwamba mfungwa wa sita wa Guantanamo ambaye pia anatoka Algeria na alikamatwa pamoja na wenzake wengine huko Bosnia- Herzegovina hapo mwaka 2001 amekuwa akishikiliwa kwa mujibu wa sheria. Hukumu yake hiyo ya kihistoria ya kwanza katika kesi za aina yake juu ya ugaidi ilitafsiriwa moja kwa moja kwa kupitia kiungo cha simu kwa wafungwa hao sita walioko Guantanamo.

Kesi hiyo imesikilizwa baada Mahkama Kuu nchini Marekani kutowa hukumu hapo tarehe 12 mwezi wa Juni kwamba wafungwa katika kambi ya Guantanamo wana haki ya kujuwa wanashilikiwa chini ya mashtaka gani na kuna ushahidi gani dhidi yao.

Hakimu Leon amesema rufaa ya mfungwa wa sita iliowasilishwa na Belcasem Bensayah mwenye umri wa miaka 46 imekataliwa kwa sababu serikali imethibitisha kwa ushahidi mkubwa kwamba inayumkinika zaidi Bensayah alipanga kwenda Afghanistan na kurahisisha safari za watu wengine kwenda kupambana na vikosi vya Marekani jambo ambalo moja kwa moja linamaanisha kuunga mkono kundi la Al Qaeda.

Hukumu hiyo inatolewa baada ya kesi hiyo kusikilizwa kwa siku saba siki sita zikiwa za faragha.Watu hao wote sita walikuwa wakiishi Bosnia na walikuwa na uraia wa nchi mbili Bosnia na Algeria na walikamatwa mwishoni mwa mwaka 2001.

Mashtaka ya awali ya kutaka kushambulia ubalozi wa Marekani mjini Sarajevo yalifutwa lakini wakati kesi yao ilipoanza kusikilizwa hapo tarehe 6 Novemba walituhumiwa kupanga kwenda Afghanistan kupambana na vikosi vya Marekani.

Takriban wafungwa 250 wanasota katika kambi ya kijeshi ya Guantanamo ambayo imeharibu sifa ya Marekani nchi za nje na makundi ya haki za binaadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakitowa wito wa kufungwa kwa kambi hiyo ambapo Rais Mteule wa Marekani Barack Obama amesema ndio kusudio lake.

Bush na utawala wake pia wamekiri kwamba gereza hilo linapaswa kufungwa lakini kumekuwa hakuna makubaliano juu ya namna ya kuwashughulia wafungwa waliobakia wengi wao watakabiliwa na mateso na ukandamizaji watakaporudishwa makwao.