Haki za walemavu kutambuliwa ulimwenguni | Masuala ya Jamii | DW | 14.12.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Haki za walemavu kutambuliwa ulimwenguni

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hatimaye limeidhinisha makubaliano ya kimataifa ya kulinda haki za walemavu ulimwenguni.Hii inatokea baada ya majadiliano ya miaka mitano .

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa

Nchi 192 wanachama zitatia saini makubaliano hayo na kuyathibitisha mwezi machi mwaka ujao.Takriban asilimia 10 ya watu ulimwenguni wanaishi na ulemavu wa aina fulani.Kulingana na maafisa wa Umoja wa Mataifa idadi hiyo inaongezeka.

Kulingana na Wanadiplomasia kutoka mataifa kadhaa makubaliano hayo ni hatua kubwa kwa watu wanaoishi na ulemavu kwani haki zao hazitapuuzwa au kutotimizwa kote ulimwenguni.

Watetezi wa makubaliano hayo wanashikilia kuwa japo walemavu wana haki kama za wengine kimsingi,katika maisha ya kawaida wanatengwa katika nyanja mbali mbali kama vile nafasi za kazi,elimu na hata huduma za afya.

Hata hivyo mataifa yanatarajiwa kuunda mikakati itakayowezesha walemavu kuishi kama watu wengine na kupata nafasi sawa katika huduma za usafiri,elimu,nafasi za kazi na hata starehe.Hii haimaanishi kwamba mataifa yanapaswa kuchukua hatua ambazo haziwezi kugharamia.

Kwa sasa mataifa 45 pekee ndio yanakubali na kufata sheria zinazohusu haki za walemavu.Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa.Utekelezaji ni jambo nyeti ili makubaliano hayo yatimizwe.

Baraza hilo aidha limekubali itifaki za mawasiliano zinazowaruhusu watu binafsi vilevile makundi kutoa malalamiko kwa Kamati inayohusika na Haki za Walemavu endapo hatua nyingine zinashindwa kupata suluhu.

Maafisa hao aidha kamati hiyo inayowahusisha wataalam binafsi itazinduliwa rasmi baada ya makubaliano hayo kuanza kutimizwa.Vilevile kamati hiyo itapokea ripoti kuhusu hatua zinazopigwa katika utekelezaji.

Makubaliano hayo yanaeleza kwamba walemavu sharti waweze kuishi maisha kama ya watu wengine kwa usawa….wapate haki sawa vilevile nafasi za kuimarisha maisha yao hasa wanawake na watoto.Mataifa husika yatapaswa kutambua kuwa watu wote ni sawa kisheria aidha kupiga marufuku ubaguzi kwasababu ya ulemavu.

Benki ya Dunia inakisia kuwa asilimia 20 ya watu masikini zaidi ulimwenguni wana ulemavu na aghalabu wanakosa nafasi sawa katika jamii hasa wanawake na watoto wa kike wana uwezekano mkubwa wa kunyanyaswa na kufanyiwa ukatili.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto linakisia kuwa asilimia 90 ya watoto walio na ulemavu katika mataifa yanayoendelea hawaendi shule.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa ukatili dhidi ya watoto walio na ulemavu unatokea zaidi ikilinganishwa na watoto wasio na ulemavu.Vilevile aghalabu watoto hao hawapati usaidizi wa polisi,kisheria au hata mazingira yanayowalinda kutokana na vitendo vya ukatili.Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa yatakapoidhinishwa na takriban mataifa 20.

 • Tarehe 14.12.2006
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHlu
 • Tarehe 14.12.2006
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHlu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com