1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hadi watu 70 wauawa katika machafuko ya waumini wa Kala Kato

30 Desemba 2009

Hadi watu 70 wameuawa na zaidi ya 1,000 wengine wamepoteza makazi yao baada ya mapambano makali kuzuka kati ya vikosi vya usalama na waumini wa madhehebu ya Kala Kato katika mji wa Bauchi, kaskazini ya Nigeria.

https://p.dw.com/p/LH31
Karte von Nigeria mit den eingezeichneten Provinzen Yobe und Borno, der Stadt Bauchi und der Hauptstadt Abuja --- DW-Grafik: Peter Steinmetz
Ramani ya mji mkuu mkuu wa Nigeria Abuja, mji wa Bauchi na majimbo ya Yobe na Borno kaskazini ya nchi.Picha: DW

Mapigano hayo kwanza yalizuka siku ya Jumatatu, kati ya makundi mawili hasimu ya Kiislamu ya madhehebu ya Kala Kato katika mji wa Bauchi. Vikosi vya polisi viliingilia kati, mapigano yaliposhika kasi na wenyeji walipoanza kukimbia makwao.

Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la AFP alietembelea nyumba ya maiti katika mji huo, yeye alihesabu maiti 42 zilizokuwa zimepangwa sakafuni na zote zilikuwa na majeraha ya risasi au mapanga. Maiti zingine 25 ziliwekwa katika chumba kingine na nyingi zilikuwa za vijana na watoto. Polisi watatu vile vile waliuawa katika mapigano hayo.

Mapambano hasa yalichochewa na hotuba kali iliyotolewa na kiongozi wa Kala Kato, Badamasi Saleh Alkaleri. Kwa mujibu wa mkuu wa polisi, Alkaleri katika mahubiri yake alitoa wito wa kuliteketeza kundi lililojitenga na kuwaua maadui wake na yeyote yule asiefuata mwongozo wa Kala Kato. Wafuasi wake wakaanza kuwashambulia wapita njia na mahasimu wa kundi hilo lenye itikadi kali.

Polisi na vikosi vya usalama viliingilia kati kutuliza machafuko hayo katika eneo hilo wanakoishi wafuasi wengi wa madhehebu ya Kala Kato yanayojulikana pia kama Maitatsine. Vikosi hivyo vilifanikiwa kutuliza ghasia lakini Alkaleri na baadhi ya wafuasi wake waliuawa. Nyumba yake sasa imezingirwa na polisi na wanajeshi wanaojaribu kuuzuia umati wa watu wenye hasira uliokusanyika katika eneo hilo.

Uasi uliofanywa na waumini wa madhehebu ya Kala Kato katika mwaka 1980 katika mji wa kaskazini wa Kano ulisababisha vifo vya maelfu ya watu na tena katika mwaka 1992, maelfu wengine waliuawa pale machafuko yalipozuka katika mji mkuu wa jimbo la Adamawa huko huko kaskazini mwa Nigeria.

Madhehebu ya Kala Kato yanapinga cho chote cha kisasa, ikiwa ni pamoja na elimu ya magharibi na matumizi ya dawa. Vile vile waumini wake hawaruhusiwi kuwa na televisheni na redio majumbani mwao wala vitabu vya aina yo yote ile isipokuwa Quran Takatifu.

Madhehebu hiyo imekuwa ikifuatwa tangu miongo kadhaa katika majimbo mengi ya kaskazini nchini Nigeria. Idadi ya wafuasi wake haijulikani lakini inatathminiwa kufikia maelfu kadhaa.

Mwandishi: Martin,Prema/DPAE/AFPE

Mhariri: Othman, Miraji