1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aonyo kuhusu uwezekano wa vita vya Syria kutanuka

John Juma
13 Aprili 2018

Antonio Guterres asema hali katika Mashariki ya Kati imekuwa tete na ni tishio la usalama na amani ulimwenguni. Amewataka wadau wote katika mgogoro wa Syria kuwajibika kwa njia ipasavyo

https://p.dw.com/p/2w1MP
USA UN-Sicherheitsrat 2000 - Resolution 1325
Picha: picture alliance/Pacific Press/L. Rampelotto

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mkwamo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria unazidisha taharuki inayotishia uwezekano wa kutokea kwa vita vya kijeshi. Baraza hilo linakutana leo kufuatia ombi la Urusi katika juhudi za kutafutia ufumbuzi mkwamo ulioko.

Akihutubia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amezitaka pande zote kuwajibika ipasavyo kuhusu vita vya Syria ili kuepuka kutokea kwa vita. Guterres amesema nguvu ya kijeshi haiwezi kuwa suluhisho la vita. Wito wa Guterres unajiri wakati Marekani, Uingereza na Ufaransa zikitafakari kutumia nguvu za kijeshi kuiadhibu Syria kufuatia madai kwamba ilifanya mashambulizi kutumia silaha za sumu. Guterres ameendelea kusema:

"Masharti kuhusu silaha za sumu sharti yafuatwe. Ni wajibu wetu kuhakikisha uwajibikaji katika shambulizi la sumu ambalo limethibitishwa hata kwa waathiriwa wa mashambulizi hayo. Kutowawajibisha wanaofanya mashambulizi hayo ni kuwapa uhakikisho wa kuendelea kuvunja sheria bila kujali. Hali ambayo baadaye hulegeza sheria kuhusu silaha hizo za sumu. Ninawahimiza wadau wote kuwajibika vyema kwa kila namna katika hali hizi za hatari."

Wanajeshi wa Urusi wakiwa karibu na mji wa Douma 12.04.2018
Wanajeshi wa Urusi wakiwa karibu na mji wa Douma 12.04.2018Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Memeri

Katika tukio linalofungamana na suala la syria, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi ina ushahidi usiopingika kwamba madai ya shambulizi kutumia silaha za sumu ni njama tu iliyopangwa kwa usaidizi wa majasusi kutoka nchi nyingine.

Macron na Putin wazungumza

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin nao wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu kuhusu hali ya Syria. Macron amemuelezea Putin kwamba amesikitishwa na hatua ya Urusi kutumia kura yake ya turufu kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa la kutaka uchunguzi wa kimkakati dhidi ya mashambulizi kama ya Syria. Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya mkutano mwengine tena kuhusu Syria kuhusu kufuatia ombi la Urusi.

Hayo yanajiri wakati wachunguzi wa shirika linalodhibiti silaha za sumu wakitarajiwa kuwasili Syria na kuanza uchunguzi wao kesho. Huku kukiwa na hofu ya uwezekano wa Marekani na washirika wake kushambulia Syria kufuatia madai kwamba ilifanya shambulizi kwa kutumia silaha za sumu, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameonya leo kuwa kuingiliwa kokote kwa Syria nanchi za magharibi kutasababisha wimbi jipya la wahamiaji kuelekea Ulaya.

Jamaa aomboleza kufuatia vifo vya watu 75 miongoni mwao kina mama na watoto mjini nchini Syria baada ya shambulizi lililodaiwa kufanywa kutumia silaha za sumu
Jamaa aomboleza kufuatia vifo vya watu 75 miongoni mwao kina mama na watoto mjini nchini Syria baada ya shambulizi lililodaiwa kufanywa kutumia silaha za sumuPicha: picture-alliance/newscom/M. Hassan

Ujerumani yataka Urusi kuongezewa shinikizo

Kwa upande mwengine, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema ni sharti nchi za magharibi ziongeze shinikizo dhidi ya Urusi kuhusu majukumu yake katika vita vya Syria. Maas ameonya kuwa matumizi ya silaha za sumu hayawezi kuachwa tu bila jibu.

Baada ya mazungumzo na mkuu wa halmashauri kuu  ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker, Heiko Maas ameishambulia Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa rais wa Syria Bashar al-Assad, kwa kuzuia mara kwa mara maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria.

"Matumizi ya mara kwa mara ya silaha za sumu ambazo zimepigwa marufuku kimataifa hayawezi kuendelea bila adhabu. Huwezi kuendelea tu na ajenda. Hilo ndilo suala ambalo sharti tujadili pamoja na wenzetu kutoka nchi za Magharibi. Lengo lazima liwe ni kuafikia suluhisho la kisiasa. Hakutakuwa na suluhisho la kudumu Syria bila ya suluhisho la kisiasa."

Mjini Ankara ,Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan naye amesema amefanya mazungumzo kadhaa wiki hii kwa simu na Rais Donald Trump pamoja na Rais Putin na amehimiza kuwepo utulivu na juhudi za kurejesha Amani, na kwamba kwa sasa taharuki iliyokuwepo kati ya nchi hizo mbili kuhusiana na shambulizi la Syria linalodaiwa kuwa la sumu imepungua.

Mwandishi: John Juma/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman