1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guru ahukumiwa kifungo India

Sekione Kitojo
28 Agosti 2017

Jaji  wa mahakama nchini  India amemhukumu, mtu aliyejitangaza kwamba ni Mungu, ambae  wafuasia wake walifanya ghasia baada  ya kuhukumiwa kwa ubakaji wiki iliyopita, na kuamriwa kwenda  jela  miaka 10 leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/2izKr
Gurmeet Ram Rahim
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Topgyal

Lakini  amri  ya kumfyatulia risasi  mtu yeyote na kumuua, kutotembea  usiku  na polisi  wengi kuwekwa  katika  eneo  hilo kuliwazuwia  waandamanaji kufanya ghasia zaidi  baada ya  hukumu  hiyo.

Mamia  kwa  maelfu ya  polisi  waliimarisha usalama  na  kulifunga eneo  kubwa  la  jimbo  la  kaskazini  la  Haryana  na  Punjab ambako  Gurmeet Ram Rahim Singh, mwenye  umri  wa  miaka  50 , ana  wafuasi  wengi.

Indien Panchkula - Ausschreitungen Unterstützer des religiösen Führers Gurmeet Ram Rahim Singh
Wafuasi wa Guru wakifanya ghasia na uharibifuPicha: Getty Images/AFP/M. Sharma

Polisi  katika  jimbo  la  Haryana wametoa  amri  kupiga  risasi waandamanaji  wanapowaona  kabla  ya  kutolewa  hukumu  na polisi  imeamuru  kesi  hiyo  kufanyika  nje  ya  jela  ambako  Singh anashikiliwa.

Mamia  ya  wafuasi walifanya  ghasia  wakati  alipohukumiwa  siku ya  Ijumaa, wakishambulia  vituo  vya  treni, mabasi  na  magari  ya televisheni.

Kiasi  watu 38 waliuwawa  na  zaidi  ya  200  walijeruhiwa , na kusababisha  ukosoaji  kwamba  chama  tawala  cha  waziri  mkuu Narendra  Modi , ambacho  pia  kinatawala  katika  jimbo  la Haryana , ama  hakina uwezo ama  hakitaki  kuchukua  hatua  dhidi ya  wafuasi  wa  Singh.

Indien Panchkula
Walichoma magari na kufanya uharibifu mkubwaPicha: picture-alliance/AP Photo/A.Qadri

Singh ashutumiwa kwa ubakaji

"Mahakama imeamuru mshitakiwa  afungwe  miaka  10 jela,"  Ram Niwas , mtaalamu  anayehusika  na  masuala  ya  sheria  na  utulivu katika  jimbo  la  Haryana , ameliambia  shirika  la  habari  la Reuters.

Kesi  hiyo  ni  ya  tangu  mwaka  2002 wakati  wanawake  wawili wafuasi  wake  walipomshutumu Singh  kwa  ubakaji  katika  makao makuu  ya jumuiya  yake  ya  Dera Sacha sauda  katika  mji  wa Sirsa.

Singh , ambaye  pia  anafahamika   kama  guru  wa  vito vya thamani  na  nguo , kutokana  na  nguo  na  vito anavyovaa katika filamu  anazozitayarisha  mwenyewe, anakabiliwa  na  kifungo  cha miaka  saba  chini  ya  sheria  mpya  ngumu  za  ubakaji.

Indien Nirankari Baba Hardev Singh
Wafuasi wa kiongozi wa kiroho Singh nchini IndiaPicha: Getty Images/AFD/N. Nanu

Wakili  wa  Singh , A.K. Panth , amesema  mteja  wake hana  hatia na  atakata  rufaa. Vipassana Insaan , msemaji  wa  Dera sacha sauda , amewataka  wafuasia  wa  Singh  kuheshimu  amri  ya mahakama.

"Mapambano  yetu  ya  kisheria  hayatamalizika  hapa. Mteja  wetu hana  hatia  kabisa,"  amesema  Panth.

Aahidi  kukata rufaa

Vituo  vya  televisheni  nchini  India  vimeripoti  kwamba  Singh alifadhaika  sana  baada  ya  hukumu  kupitishwa  na  kukataa kusogea  na  kutoka  nje  ya  chumba  cha  mahakama, akisema hana  hatia.

Jela  katika  mji  wa  Rohtak , kilometa  66  kutoka  New Delhi, iligeuzwa  kuwa  ngome, ambapo  waandishi  habari  waliopigwa marufuku  kukaribia  eneo  hilo kwa  umbali  wa  kilometa  1.6 na barabara  ziliwekwa  uzio  wa  waya.

V. Umashankar , kamishna  maalum   katika  jimbo  la  Haryana , amesema  marufuku  ya  kutembea  ovyo  inaendelea  katika  mji  wa Sirsa  na  maeneo  ya  Rohtak.

Kuhukumiwa  kwa  Singh  katika  kesi  ya  ubakaji  ni  ya  hivi karibuni  katika  mlolongo  wa  kesi zinazohusisha  viongozi  wa kiroho  ambao  wamekuwa  wakishutumiwa  kwa  kuwadhalilisha kingono  wafuasi  wao, wakijilimbikia  fedha  ambazo  hazotozwi  kodi na  kupata  ushawishi  wa  wanasiasa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman