1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gul akutana na Merkel

20 Septemba 2011

Rais Abdullah Gul wa Uturuki ameendelea na ziara yake hii leo (20.09.2011) nchini Ujerumani kwa kumtembelea Kansela Angela Merkel kwenye makao yake makuu jijini Berlin, huku huko mjini Ankara kukitokea mashambulizi.

https://p.dw.com/p/12cw6
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Abdullah Gul wa Uturuki
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Abdullah Gul wa UturukiPicha: picture-alliance/dpa

Kansela Merkel ameitumia nafasi hii ya kukutana na Rais Gul kuzungumzia wasiwasi wa Ujerumani kwa mgogoro wa kidiplomasia uliopo kati ya Uturuki na Israel, wote washirika muhimu wa kibiashara na kisiasa wa Ujerumani.

Kiasi ya Waturuki milioni tatu na nusu wanaishi nchini Ujerumani, jambo ambalo linawafanya kuwa kundi kubwa kabisa la wachache kuishi katika nchi barani Ulaya.

Mgogoro kati ya Uturuki na Israel ulianzia kwenye mkasa wa mashambulizi ya makamando wa Israel dhidi ya watu waliokuwa kwenye msafara wa meli zilizokuwa zikielekea Gaza, hapo mwezi Mei mwaka jana, ambapo raia kadhaa wa Uturuki waliuawa.

Vyanzo vya habari kutoka makao makuu ya Kansela Merkel, vinasema kwamba viongozi wote wawili, walionesha tafauti zao juu ya uwanachama wa Uturuki kwa Umoja wa Ulaya.

Hapo jana Rais Gul alirejelea msimamo wake kuwa nchi yake itaendelea kupigania uwanachama kamili wa Umoja huo.

Kimsingi, Ujerumani haipingani na wazo la Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini chama cha Christian Democrat cha Kansela Merkel kinataka Uturuki kisiwe na nafasi kubwa zaidi ya ushirikiano kwenye Umoja wa Ulaya.

Baada ya kukutana na Kansela Merkel, Rais Gul alitembelea mji wa Osnabrück, nyumbani kwa Rais wa Ujerumani, Christian Wulff, ambaye naye aliwahi kutembelea mji aliozaliwa Rais Gul wa Kayseri, hapo mwaka jana. Rais Wull aliyaelezea mahusiano kati ya Ujerumani na Uturuki kuwa ni mazuri

"Tunapitia katika kipindi ambacho tunakubaliana katika masuala mengi, na tumefikia mapatano mengi, ambayo hatujawahi kuwa nayo hapo kabla". Amesema Rais Wulff.

Kwengineko nchini Uturuki kwenyewe, kumetokea mripuko mkubwa wa bomu kwenye mji mkuu Ankara, ambapo watu watatu wameuawa na wengine 15 kujeruhiwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Idris Naim Sahin, amesema kwamba washukiwa wa kwanza wa mashambulizi haya ni chama cha Kikurdi kinachopigania kujitenga, PKK. Waziri Sahin amesema kwamba hali za majeruhi watano ni mbaya sana.

Akiwa ziarani nchini Ujerumani, Rais Gul ameyalaani mashambulizi haya kwa kuyaita kuwa ni "ya kinyama".

Bomu hilo lililoripuka nje ya ofisi za serikali katika wilaya ya Cankaya, lilivivurumisha vioo vya madirisha katika maduka na maofisi, kuharibu magari na kuzusha moto mkubwa, ambao baadaye ulizimwa na vikosi vya uokozi.

Ofisi zilizoshambuliwa ziko karibu na uwanja wa Kizilay kwenye mji wenye wakaazi milioni nne, ambapo yapo pia makao makuu ya jeshi la Uturuki.

Mashambulizi haya yamekuja siku chache tu baada ya Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kusema kuwa nchi yake ilikuwa tayari kuanzisha mashambulizi ya ardhini dhidi ya makambi ya waasi wa PKK, mpakani mwa nchi hiyo na Iraq.

Serikali ya Uturuki imekuwa ikifikiria hatua kadhaa za kuchukuwa kukabiliana na wimbi la mashambulizi kutoka PKK, ikiwemo la kuliomba Bunge kurefusha muda wa operesheni za kijeshi kwenye eneo hilo kwa mwaka mmoja zaidi. Muda wa sasa unamalizika mwezi ujao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman