1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guido Westerwelle afariki dunia

18 Machi 2016

Westerwelle ameaga dunia leo (18.03.2016) akiwa na umri wa miaka 54 na amekuwa akiugua saratani ya damu tangu Juni 2014. Alikuwa waziri wa mambo ya nje 2009 hadi 2013 na naibu kansela wa Ujerumani 2009 hadi 2011.

https://p.dw.com/p/1IFsk
Guido Westerwelle ehemaliger Bundesaußenminister
Picha: picture-alliance/dpa/K. Schindler

"Tunaomboleza kifo cha kiongozi wetu Guido Westerwelle," umesema wakfu wake katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook. Amekufa Machi 18, 2016 katika hospitali ya chuo kikuu cha Cologne kutokana na matamizo yaliyosababishwa na matibabu dhidi ya ugonjwa wa saratani ya damu, leukemia."

Westerwelle, alikuwa waziri wa mambo ya nje kuanzia 2009 hadi 2013 na akawa naibu kansela wa Ujerumani katika serikali iliyopita ya Angela Merkel kuanzia 2009 hadi 2011.

Mkuu wa afisi ya Westerwelle katika wakfu wa Westerwelle, Alexander Vogel, amethiitisha kifo cha waziri huyo wa zamani akisema amekufa leo Ijumaa lakini hakutoa maelezo zaidi.

Kama waziri wa mambo ya nje Westerwelle alipigania sana utamaduni wa kutotumia hatua za kijeshi na alipinga hatua ya jumuiya ya NATO kujiingiza kijeshi nchini Libya 2011. Alikuwa waziri na naibu kansela 2009 baada ya kukiongoza chama chake cha Free Democratic, FDP, kupata matokeo mazuri kabisa katika uchaguzi na kuufikisha kikomo muda wa miaka 11 wa kukaa upande wa upinzani.

Waziri huyo alijiuzulu kutoka siasa Desemba mwaka uliopita baada ya chama chake kinachopendelea biashara, Free Democratic, FDP, kupoteza viti vyote vya ubunge.

Deutschland Bundestag 2009 Angela Merkel & Guido Westerwelle
Guido Westerwelle, kulia, na kansela Angela Merkel, bungeni (28.10.2009)Picha: Getty Images/A. Rentz

Akiwa mwanasiasa mwenye kipaji na kiongozi wa upinzani, Westerwelle aliwavutia wapigaji kura kwa ahadi zake za kupunguza kodi kwa kiwango kikubwa. Lakini hakuweza kuzitimiza ahadi hizo baada ya kuingia katika serikali ya Merkel na umaarufu wa chama chake kuporomoka kwa kulaumiwa kwa malumbano ya ndani ya serikali ya mseto.

Hata Ujerumani ilipoonyesha utayarifu wake kushinikiza uwezo wake mkubwa kiuchumi wakati bara la Ulaya lilipokabiliwa na mgogoro wa madeni, Westerwelle aliimarisha utamaduni wa nchi yake kusita kuburuzwa katika harakati za kijeshi katika mataifa ya kigeni.

Mwaka 2011 Ujerumani iliamua kupinga harakati ya kijeshi ya jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Libya na pia ikasita kupiga kura ya baraza la usalama iliyoidhinisha harakati hiyo, hatua ambayo iliiweka Ujerumani katika upinzani na nchi za magharibi ambazo ni washirika wake.

Wakati alipokuwa uongozini, Ujerumani ilishiriki mazungumzo ya pande sita na Iran kuhusu mzozo wake wa nyuklia yaliyosaidia kupatikana mkataba wa awali ulioshuhudia Iran ikisitisha urutubishaji wa madini ya urani na baadhi ya shughuli za mpango wake wa nyuklia ili ilegezewe vikwazo.

Barani Ulaya Westerwelle aliunga mkono muelekeo wa Merkel katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa madeni, ingawa alielezea wasiwasi wake juu ya kauli za baadhi ya wanasiasa wa pande zote mbili za mzozo huo. "Lazima tuwe waangalifu kauli zetu zisiiangushe Ulaya," alisema Westerwelle wakati wa kilele cha mzozo wa madeni mwaka 2012.

Mwandishi:Josephat Charo/dpa/afpe

Mhariri:Saumu Yusuf