1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Goma: Tembo Vwira na kampuni ya kuzoa taka

16 Juni 2015

Mji wa Goma unajulikana duniani kuwa mahala pa vita na maafa ya wakimbizi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Lakini licha ya hali hiyo kijana mmoja ameanzisha kampuni ya kuzoa taka katika mji huo.

https://p.dw.com/p/1FhqO
Der Müllunternehmer von Goma
Picha: DW/J. Raupp

Joel Tembo Vwira aliianzisha kampuni yake Business and Services miaka saba iliyopita katika jiji la Goma, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Jiji hilo lipo katika jimbo linalojulikana kwa migogoro iliyochukua muda wa miaka takriban zaidi ya 20. Migogoro hiyo huripuka mara kwa mara.

"Kilichonivutia hasa, na kile nilichokiona kama changamoto ni suala la usafi, na hasa ukosefu wa mfumo wa kuondoa taka. Kabla ya mwaka wa 2008 kila mmoja alitupa taka popote pale. Katika sehemu kama kwenye makutano ya barabara au kwenye mitaa mikubwa palijaa majalala.Hali hiyo ilinikasirisha", anakumbuka mmiliki wa kampuni hiyo ya kuzoa taka, Business and Services.

Der Müllunternehmer von Goma
Picha: DW/J. Raupp

Ubalozi wa Marekani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa waliomsifu kijana huyo alienzisha kampuni ya kuzoa taka. Kutokana na mpango wa Marekani wa kuwasaidia wajisiriamali wanaochipukia barani Afrika, Joel Tembo aliweza kupata fursa ya kuitambulisha kampuni yake kwa kampuni na wataalamu wa nchini Marekani kwa muda wa miezi miwili. Na kote alikoenda kijana huyo alipewa pongezi.

Lakini nyumbani katika jiji la Goma, Joel Tembo kwa sasa anawasiliana na watu wanaojiweza kifedha. Malipo kwa jili ya huduma ya kuondolewa taka ni dola 11 kwa mwezi. Kiasi hicho ni kikubwa kwa watu wengi katika jiji la Goma. Hata hivyo wakaazi wengi wa jiji hilo wanaithamini kazi anayoifanya kijana huyo. Sababu ni kwamba usafi ni msingi mmojawapo muhimu wa kudumisha afya katika jamii.

Mkaazi mmoja, Annie Muyisa ambae ni daktari amesema: "Kutokana na huduma ya kuzoa taka sasa tunaweza kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi. Ni muhimu sana hasa kwa watoto. Ikiwa watu wanaishi katika sehemu ya kubanana, na ikiwa uchafu hauondolewi, hali hiyo inasababisha matatizo." Mkaazi mwengine wa jiji la Goma, Anita Kapitula amesema, katika vitongoji vya masikini, watu wanazichoma moto taka ili kuwaepusha na maradhi watoto na watu wengine.

Der Müllunternehmer von Goma
Picha: DW/J. Raupp

Wafanyakazi wa Joel Tembo wanapitia kwenye njia zenye mabonde bonde ili kupeleka taka hadi kwenye jaa kubwa. Hapo ni mahala ambapo taka huchujwa. Ni umbali wa kilometa 20 kutoka Goma mjini. Asilimia 70 inatokana na mboji ambayo Tembo anaiuza kwa wenye bustani. Kampuni ya Joel Tembo inaingiza mapato ya dola karibu alfu 60 kwa mwaka.

Lakini mjasiriamali huyo bado hajatosheka na kapumpuni ya kuzoa taka tu. Sasa anakusudia kuanzisha kiwanda cha kuzifanyia taka ukarabati kama jinsi inavyofanyika barani Ulaya. Lakini kwa ajili hiyo anhitaji mtaji wa dola milioni moja na nusu. Baadhi ya watu wanafikiri kuwa anaota ndoto tu. Lakini Joel Tembo tayari anafanya mazungumzo na washirika. Amesema kwamba anafanya mazungumzo na kitengo cha ulinzi wa mazingira cha Umoja wa Mataifa pamoja na wawakilishi wa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.

Joel Tembo anatumai kwamba serikali ya jimbo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itapitisha sheria ya usafi itakayowawajibisha watu wote,na katika kila kaya ,kuondoa uchafu kwa namna inayostahili.

Mwandishi: Raupp Judith

Tafsiri: Mtullya Abdu

Mhariri: Mohammed Khelef