1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GHAZNI:Taleban wasema huenda wakawaachia mateka wa Korea Kusini muda mfupi ujayo

11 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBaA

Viongozi wa kundi la Taleban wanaoshiriki katika mazungumzo ya majaaliwa ya mateka 21 raia wa Korea Kusini wanaoshikiliwa na wanamgambo hao, wamesema kuwa huenda mateka hao wakaachiwa leo ama kesho.

Mullah Qadri Bashir ambaye ni mmoja wa viongozi hao amesema kuwa mazungumzo ya ana kwa ana na maafisa wanne wa Serikali ya Korea Kusini yaliyoanza jana yanaendelea vizuri na kwamba bado hata hivyo wanashikilia kutimizwa kwa matakwa yao.

Taleban wanadai kuachiwa kwa wenzao 21 waliyoko katika magereza ya Afghnaistan.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za shirika la msalaba mwekundu mjini Ghazni kunakofanyika mazungumzo hayo, Mullah Bashir amesema kuwa kwa uwezo wa mwenyezi mungu Serikali za Korea Kusini na Afghanistan zitakubaliana na matakwa yao.

Kundi la Taleba liliwateka Raia hao wa Korea Kusini ambao ni wafanyakazi wa kujitolea, mwezi mmoja uliyopita, ambapo tayari limekwishawaua mateka wawili.