1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GHAZNI : Operesheni ya kuokowa mateka yaanza

1 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBd7

Operesheni ya kijeshi kuwaokowa mateka 21 wa Korea Kusini waliobakia ambao wanashikiliwa na waasi wa kundi la Taliban nchini Afghanistan imeanza leo hii masaa machache baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho uliowekwa na Taliban kutimiziwa madai yao na serikali ya kuachiliwa kwa wafungwa wao wanane walioko magerezani.

Hayo yamesemwa na Khowja Seddique mkuu wa wilaya ya Qarabagh katika jimbo la Ghazni ambapo Taliban iliwateka wafanyakazi wa Kikristo wa kujitolea wa Korea Kusini karibu wiki mbili zilizopita.

Hakutowa maelezo zaidi au kusema ni vikosi gani vinavyohusika na operesheni hiyo.

Taliban kundi la itikadi kali za Kiislam limekuwa likionya mara kadhaa kwamba matumizi yoyote yale ya nguvu yatahatarisha maisha ya Wakorea hao 18 wanawake na wanaume watatu ambao wamewagawa katika makundi madogo na kuwashikilia katika maeneo tafauti.Kundi hilo tayari limewauwa mateka wawili wa Korea.

Mapema jeshi lilidondosha vipeperushi kuwaonya raia juu ya shambulio linalokuja.

Wakati huo huo maafisa wa serikali ya Ujerumani wameyakinisha leo hii kwamba haitokubali shinikizo kutoka Taliban kuwaondowa wanajeshi wake kutoka Afghanistan baada ya televisheni ya kituo cha Al Jazeera hapo jana kurusha ukanda wa video wenye kuonyesha mateka wa Ujerumani.

Peter Struck kiongozi wa bunge wa chama cha mrengo wa kulia wa wastani Social Demokratik ambacho kinaunda serikali ya mseto na wahafidhina wa chama cha Kansela Angela Merkel amesema hawawezi kusalimu amri kutokana na madai hayo.

Waziri huyo wa zamani wa ulinzi Struck amesema hakuna suala la kuwaondowa wanajeshi 3,000 wa Ujerumani walioko kusini mwa Afghanistan.

Mjerumani alietambulika kwa jina la Rudolh B ameonekana kwenye ukanda huo akiziomba Ujerumani na Marekani kuondowa wanajeshi wao kutoka Afghanistan kusaidia kuokowa maisha yake.

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema wataalamu wanauchunguza ukanda huo ambao unaonyesha mmojawapo ya wanamgambo wakimuelekezea zana ya kuvurumishia roketi mateka huyo wa Kijerumani.