Ghasia zazuka Mombasa baada ya kuuawa Aboud Rogo | Matukio ya Afrika | DW | 28.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Ghasia zazuka Mombasa baada ya kuuawa Aboud Rogo

Mji wa Mombasa nchini Kenya umekumbwa na vurugu kufuatia kuuawa kwa mhubiri wa dini ya Kiislamu Aboud Rogo Mohammed, ambaye alihusishwa na makundi ya Kigaidi.

Ghasia mjini Mombasa

Ghasia mjini Mombasa

Mamia ya vijana wenye hasira walifanya vurugu katika mji wa Mombasa, wakirusha mawe na kuharibu magari huku wakielekea katikati ya mji huo. Machafuko hayo ni mwendelezo wa yale yaliyozuka Jumatatu, mara baada ya kuuwawa kwa mhubiri Aboud Rogo, ambaye kwa mujibu wa polisi alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana. Rogo alikuwa katika orodha ya watu waliowekewa vizuizi na Marekani na Umoja wa Mataifa kwa tuhuma za kuliunga mkono kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Aboud Rogo alipokuwa katika mahakama kuu jijini Nairobi

Aboud Rogo alipokuwa katika mahakama kuu jijini Nairobi

Makundi ya Waislamu yameishutumu polisi kwa kifo cha Rogo. Hata hivyo, polisi imekanusha madai hayo na kusema kwamba juhudi za kuwasaka waliomuuwa Rogo bado zinaendelea. Kituo cha vijana wa kiislamu, kilichokuwa kikiongozwa na Rogo, kimetoa tamko lake na kusema kwamba Rogo ameuliwa na "makafiri" katika mpango wa polisi wa kuwauwa viongozi maarufu wa Kiislamu nchini Kenya.

Al-Shabaab yawataka waislamu waungane

Kituo cha vijana wa Kiislamu kimeelezea kuuwawa kwa Rogo kuwa kitendo cha kinyama na kimeonya kwamba kinaulaumu uongozi wa Kenya kwa kuuwawa kwa kiongozi huyo.

Kupitia taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa twitter, kundi la waasi la al-Shabaab limewataka waislamu nchini Kenya wachukue hatua zote ziwezekanazo kuilinda dini yao na kuususia uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2013. Kundi la al-Shabaab limeeleza kwamba ni muhimu kwa waumini wa dini ya Kiislamu kuilinda dini yao na vile vile heshima yao, mali zao na maisha yao dhidi ya wale walioitwa maadui wa dini ya Kiislamu.

Mgogoro wa kidini waibuka

Waandamanaji walivamia magari na majengo mjini Mombasa

Waandamanaji walivamia magari na majengo mjini Mombasa

Waandamanaji mjini Mombasa walivamia makanisa mawili na kujaribu kuyachoma moto. Samani zilishika moto na baadaye moto huo uliweza kuzimwa kabla ya makanisa hayo kuungua kabisa. Makanisa yasiyopungua manne yalivamiwa na viti vilivyokuwa ndani kuvunjwa.

Kwa muda mrefu, uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu nchini Kenya umekuwa mzuri. Mkuu wa polisi wa mjini Mombasa, Kipkemboi Rop, ameeleza kwamba vijana walioshambulia makanisa walifanya hivyo kama jambo la ghafla na bila kufikiria. Naye Sheikh Juma Ngao, ambaye ni kiongozi wa kidini, amesema: "Vijana waliovamia makanisa labda walidhani kwamba aliyemuuwa Rogo lazima alikuwa mtu ambaye si Muislamu. Kwao, watu ambao si Waislamu ni Wakristo." Sheikh Ngao alikiri kwamba uvamizi huo ulielekezwa kwa kundi lisilohusika.

(Kusikiliza mahojiano baina ya Daniel Gakuba na kamanda wa polisi katika mkoa wa pwani, Agrey Adoli, bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini)

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/Reuters
Mhariri: Josephat Charo