1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia baada ya kupatikana mwili wa kijana wa Palestina

Mjahida2 Julai 2014

Raia wa Palestina wamepambana na wanajeshi wa Israel mjini Jerusalem baada ya kugunduliwa mwili wa kijana mmoja wa kipalestina huku zikijitokeza tuhuma kwamba mauaji hayo ni ya kulipiza kisasi

https://p.dw.com/p/1CUOd
Kijana wa kipalestina akipeperusha bendera ya nchi hiyo
Kijana wa kipalestina akipeperusha bendera ya nchi hiyoPicha: SAIF DAHLAH/AFP/Getty Images

kijana huyo anasemekana kuuwawa na wanajeshi wa Israel katika hatua ya kulipiza kisasi mauaji ya vijana watatu waliotekwa nyara na kuuwawa na kundi la wapalestina la Hamas.

Kulingana na wakaazi wa eneo la Shuafat mjini Jerusalem, waliozungumza na shirika la habari la Reuters walimuona kijana mmoja kwa jina Mohammed Abu Khudair aliye na Umri wa miaka 16, akilazimishwa kuingia ndani ya gari nje ya duka moja jana usiku.

Kwa upande wake Micky Rosenfeld, msemaji wa polisi nchini Israel, amesema polisi waliarifiwa juu ya kisa hicho na vizuizi vya polisi vikawekwa mara moja ili kuwatafuta na kuwakamata washukiwa.

Rosenfeld amesema baadaye polisi waliupata mwili wa kijana mmoja katika msitu wa Jerusalem na kuanza uchunguzi kujua iwapo ni wa kijana aliyeripotiwa kutekwa nyara.

Vijana wakikimbia mabomu ya kutoa machozi
Vijana wakikimbia mabomu ya kutoa machoziPicha: JAAFAR ASHTIYEH/AFP/Getty Images

Hata hivyo afisa mmoja mkuu katika chama cha Fatah cha Rais Mahmood Abbas wa palestina amesema baadaye familia ya kijana huyo waliutambua mwili, lakini hawakuweza kupatikana kwa maelezo zaidi.

Muda mfupi baada ya kupatikana mwili wa Mohammed Abu Khudair, mamia ya vijana wa kiarabu walifunga barabara ya reli ya Israel huku wakiwarushia mawe wanajeshi wa Israel waliochukua hatua ya kujibu mashambulizi kwa kufyatua hewani risasi za mipira.

Habari zaidi zinasema kwamba watu wanne wamejeruhiwa katika mashambulizi mengine yaliofanywa na Israel katika mji wa Jenin wa Palestina.

Hali ya wasiwasi yatanda katika Ukingo wa Magharibi

Aidha hali ya wasi wasi pia imetanda katika eneo la Ukingo wa Magharibi ambapo takriban wapalestina 40 walitiwa nguvuni katika msako uliofanywa kote katika ukingo huo na jeshi la Israel katika juhudi za kupambana na kundi la wapiganaji wa Hamas.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ni lazima wote waliotekeleza mauaji ya vijana watatu wa Israel wakamatwe. "Kwanza ni lazima kuwapata wauaji, na wale wote waliohusika na utekaji nyara, hatutapumzika wala hatutachoka mpaka tuwapate wote na haidhuru wapi watakapojaribu kujificha". Alisema Waziri Netanyahu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa Palestina Mahmood Abbas
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa Palestina Mahmood AbbasPicha: CHRIS KLEPONIS/AFP/Getty Images

Kwa sasa rais wa Palestina Mahmood Abbas amemtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kujitokeza wazi na kulaani mauaji ya kijana huyo wakipalestina.

Abbas mwenyewe amelaani kitendo cha kutekwa nyara na kuuwawa kwa vijana watatu wa Israel.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameshikilia msimamo wake wa kulipiza kisasi kutokana na mauaji hayo. amesema atazidisha mashambulizi ya angani dhidi ya vituo vya wapalestina katika Ukanda wa Gaza pamoja na kuzidisha operesheni za kijeshi katika ukingo wa magharibi.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu