1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghannouchi atangaza baraza jipya la mawaziri

28 Januari 2011

Kufuatia maandamano dhidi ya serikali mpya ya mpito chini ya Waziri Mkuu Mohammed Ghannouchi, sasa waziri mkuu huyo ametangaza baraza jipya la mawaziri akiwaengua mawaziri waliokuwa kwenye serikali ya Zine Ben Ali.

https://p.dw.com/p/106Qh
Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohamed Ghannouchi
Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohamed GhannouchiPicha: APImages

Bado haijawa hakika, ikiwa Ijumaa ya leo (28 Januari 2011) itapita salama, hata baada ya jioni ya jana Waziri Mkuu Ghannouchi, kutangaza mabadiliko hayo makubwa katika baraza lake la mawaziri, kwa kuwaondoa mawaziri wa ulinzi, mambo ya nje na mambo ya ndani, naye mwenyewe kurudia ahadi yake ya kuachia madaraka mara baada ya uchaguzi utakaofanyika ndani ya miezi sita ijayo.

"Hii ni serikali ya muda tu yenye dhamira moja tu na ya wazi, nayo ni kuruhusu kipindi cha mpito kuelekea demokrasia ya kweli. Jukumu lake ni kutayarisha uchaguzi. Basi!" Alisema Ghannouchi kupitia televisheni ya taifa.

Washirika wa Ben Ali waondolewa

Kamil Marjani, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje
Kamil Marjani, aliyekuwa waziri wa mambo ya njePicha: AP

Ghannouchi amemuondoa Kamil Marjani katika nafasi ya waziri wa mambo ya nje na kumuweka Ahmed Unais, ambaye ni msomi wa diplomasia na balozi wa zamani wa Tunisia katika nchi za Urusi na India.

Vile vile amemteua mwendesha mashtaka mkuu wa zamani, Farhat Rajhi, kuwa waziri wa mambo ya ndani, huku akimpa profesa wa utibabu, Abdilkarim Zebidi, wizara ya ulinzi.

Maelfu ya waandamanaji waliokaidi amri ya serikali na kuendelea kupiga kambi nje ya ofisi za Ghannouchi, walishangiria taarifa hizi, lakini wakaendelea kumshinikiza Ghannouchi naye ang'oke.

Kijana mmoja aliyebeba bango lililoandikwa "GHANNOUCHI NI KAMA BEN ALI", alisema kwamba; bado mabadiliko haya hayajafidia gharama za damu ya ndugu, jamaa na marafiki zake iliyomwagwa na utawala wa Ben Ali, ambao Ghannouchi alikuwa sehemu yake.

UGTT yapokea mabadiliko ya Baraza

Maandamano ya wanafunzi mjini Tunis
Maandamano ya wanafunzi mjini TunisPicha: AP

Chama kikuu cha wafanyakazi, UGTT, ambacho kimeshiriki kwa kiwango kikubwa katika kuung'oa utawala wa Ben Ali, kimesema hakitajiunga na serikali hii mpya, lakini kinaridhia Ghannouchi kubakia madarakani, kwa ajili tu ya kuitisha uchaguzi mpya haraka iwezekanavyo.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuridhia kwa UGTT, si lazima kumaanishe kwamba makundi yote yaliyoupinga utawala wa Ben Ali yanaunga mkono Ghannouchi kubakia madarakani, wakionya mbinu ya chama cha Ben Ali, Constitutional Democratic Rally, RCD, kujipanga tena na kurejea madarakani kwa koti la jipya.

Hata hivyo, mhadhiri katika chuo kikuu cha Tunisia, na ambaye mwenyewe alikuwa kiongozi wa UGTT, Mukhtar Aboubakar, anasema, hata kama mabadiliko haya hayajaleta manufaa makubwa, bado ni hatua kubwa mbele, kwani angalau kiwango cha ushawishi wa kaumu ya la Ben Ali, kinapotea kwa kasi.

Wapinzani wa Ben Ali warejea kutoka uhamishoni

Mpinzani wa Ben Ali, Moncef Marzouki, amerudi nyumbani kutoka Ufaransa
Mpinzani wa Ben Ali, Moncef Marzouki, amerudi nyumbani kutoka UfaransaPicha: picture alliance/dpa

Wiki iliyopita, Ghannouchi mwenyewe alijuzulu uanachama wa RCD, akijaribu kupunguza hasira za umma dhidi yake. Ndani ya kipindi cha wiki mbili zilizopita, serikali yake ya mpito imekuwa ikijaribu kuchukua hatua za kurudisha imani ya umma kwa kuondoa marufuku ya vyama vya siasa, kuwaachilia wafungwa wa kisiasa na hata kuwakamata baadhi ya wahusika wa uvunjaji wa haki za binaadamu na ufisadi, kwenye utawala ulioporomoka wa Ben Ali.

Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahdda, chenye ushawishi mkubwa nchini Tunisia, Rashid Ghannouchi, anajitayarisha kurudi nyumbani baada ya kuishi uhamishoni nchini Ufaransa kwa zaidi ya miaka 20.

Kimsingi, bado Rashid Ghannouchi ana hukumu ya kifo, aliyohukumiwa na utawala wa Ben Ali akiwa uhamishoni, lakini makumi ya wapinzani wa Ben Ali waliokuwa wakiishi nje, wamekuwa wakirudi Tunisia bila vikwazo, tangu dikteta huyo atorokee Saudi Arabia, katikati ya mwezi huu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Saumu Mwasimba