1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yamchaguwa rais

Zainab Aziz
7 Desemba 2016

Waghana wanapiga kura kumchagua rais mpya, huku tayari mgombea wa upinzani, Nana Akufo-Addo, akilalamika kuwa demokrasia nchini humo iko katika hali mbaya sana na Rais John Mahama akisema anastahiki kuendelea kuongoza.

https://p.dw.com/p/2TseW
Ghana Präsidentschaftswahlen Wahlurne
Picha: DW/K. Gänsler

Rais Mahama mwenye umri wa miaka 58 na aliyekuwa zamani makamu wa rais alichaguliwa kuwa rais mnamo mwaka 2012, baada ya kushikilia wadhIfa huo wa rais kwa miezi sita kutokana na kifo cha Rais John Atta Mills.

Ahadi ya Mahama kubwa kwenye uchaguzi huu ni kukamilisha sera yake ya uchumi na miundombinu, na kwamba kurudi kwake madarakani kuna maana kubwa kwa maisha ya wapigakura wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

 "Katika miaka minne tumeweza kuudhibiti uchumi wetu. Tumefaulu kutatua matatizo ya umeme kwa kiwango kikubwa hivyo basi miundombinu ya kijamii na kiuchumi imeimarika. Ninategemea kutawala kwa uwezo wa Mungu na raia wa Ghana ili niendeleze yale niliyokwisha yawekeza na kuinua hali zetu hadi kiwango cha kati", anasema Mahama.

Lakini Rais Mahama anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama kikuu cha upinzani, Nana Akufo-Addo, ambaye anawashawishi wapigakura kuwa kumchagua tena Mahama kutalliweka taifa hilo katika hatari siku za usoni huku akimlaumu kiongozi huyo kwa kuuongoza vibaya uchumi wa nchi hiyo hatua ambayo imewatumbukiza Waghana katika hali ngumu ya maisha. 

Mwaka 2012, Mahama alimshinda Akufo-Addo kwa kura chache katika uchaguzi huo, ambapo baadaye mgombea huyo wa chama cha upinzani aliwasilisha malalamiko yake mahakamani kupinga ushindi katika kesi iliyochukua miezi minane.

Ghana Präsidentschaftswahlen Wahlkampf
Uchaguzi wa 2016 unawakutanisha tena washindani wakubwa wa siasa za Ghana, John Mahima na Akufo-Addo.Picha: DW/K. Gänsler

Akufo-Addo pia anakilaumu chama kinachotawala cha NDC kwa kuchochea ghasia, huku polisi wakikodoa macho tu bila kuchukua hatua zozote, jambo ambalo linaitia dosari Ghana, taifa linalochukuliwa kama mwamba wa demokrasia katika bara la Afrika.

Uchaguzi wenye ushindani mkali

Wapiga kura wanatarajiwa kumchagua rais mpya kati ya wagombea saba katika kinyang'anyiro hicho cha urais ambapo pia watawachagua wabunge 275 katika uchaguzi wa leo.

Hata hivyo, hali ya wasiwasi juu ya kuvunjwa kwa demokrasia ilijitokeza kwa kiwango kikubwa wakati wote wa kampeni, huku kukiwa na malalamiko juu ya wapiga kura kutishwa pamoja na maswali juu ya uhuru wa tume ya uchaguzi.  

Ghana, nchi iliyo Afrika ya Magharibi inayouza nje dhahabu, kakao na mafuta, imewahi kuwa mfano mkubwa katika bara la Afrika kwa jinsi uchumi wake ulivyokuwa umenawiri, lakini kwa sasa imepoteza nuru yake hasa baada ya kujitumbukiza kwenye madeni.     

Tayari taifa hilo lenye wakaazi milioni 27 limeshafanya chaguzi tano tangu mwaka 1992.  chama cha NPP kimewahi kushinda  katika mwaka wa 2000 na mwaka 2004 na baadae kikashindwa na chama kinachotawala sasa cha NDC hapo 2008.

Ikizingatiwa hali ilivyo katika uchaguzi wa leo, wafuasi wengi wa chama cha upinzani wanaamini kuwa tangu mwaka wa 2000 hakuna chama kilichoweza kutwaa ushindi kwa mara tatu mfululizo, imani inayowapa tamaa kwamba mgombea wanayemuunga mkono atashinda.

Iwapo vyama vinavyochuana vitashindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura, basi duru ya pili ya uchaguzi itafanyika baadaye mwezi huu wa Desemba.  

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef