1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo azingirwa, aendelea kupambana

7 Aprili 2011

Vikosi vya Ufaransa nchini Cote d'Ivoire vimeyateketeza magari ya majeshi ya Laurent Gbagbo ili kuwaokoa maafisa wa ubalozi wa Japan, huku vikosi vya Alassane Ouattara vikiendesha operesheni kali ya kumtoa Gbagbo.

https://p.dw.com/p/10pG7
Watu waliokamatwa na vikosi vya Alassane Ouattara
Watu waliokamatwa na vikosi vya Alassane OuattaraPicha: dapd

Ingawa serikali ya Ufaransa imesema leo hii kwamba, Gbagbo ana wanajeshi wasiozidi 1,000 mjini Abdijan na 200 tu kwenye makaazi yake, hilo halijaifanya kazi ya kumtoa kwenye handaki lake wala ya kumfanya ajisalimishe na kumtambua Ouattara kama rais halali, kuwa rahisi.

Mapigano makali yameripotiwa kuendelea usiku wa kuamkia leo, kwenye makaazi ya Gbagbo na bado haijafahamika hasara iliyosababishwa na makabiliano hayo ya silaha nzito, ila inafahamika kuwa bado Gbagbo hajanaswa.

Hata hivyo, msemaji wa Ouattara, Affousy Mbamba, anasema kuwa vikosi vitiifu kwa Gbagbo havina uchaguzi mwengine zaidi ya kusalimu amri na kujiunga na Ouattara.

"Watu hawa, ambao bado wanamtii Gbagbo, hawana tena nafasi. Nataraji watang'amua kwamba mambo yamekwisha. Muda wa Gbagbo umemalizika. Watu wake pia ni raia wa Cote d'Ivoire, lazima wakiri kwamba Alassane Ouattara pia ni rais wao na wetu sote." Amesema Bamba.

Gbagbo amalizwa nguvu

Vikosi vitiifu kwa Alassane Ouattara
Vikosi vitiifu kwa Alassane OuattaraPicha: AP

Nguvu za Gbagbo zinamalizwa kutoka kila upande. Mapema leo, helikopta za kijeshi za Ufaransa ziliyateketeza magari ya kijeshi ya Gbagbo wakati wa kuwaokoa maafisa wa ubalozi wa Japan.

Hii ni baada ya majeshi ya Gbagbo kuweka mizinga ya kurushia maroketi juu ya paa la ubalozi huo na ubalozi kuomba msaada wa majeshi ya Umoja wa Mataifa na ya Ufaransa.

Huku hayo yakiendelea, hali ya maisha kwa wakaazi wa Abdijan inazidi kuwa ngumu huku wakijikuta kukwama katikati ya milio ya risasi na mizinga.

Wageni wanajaribu kuukimbia mji huo, lakini wenyeji wanalazimika kujifungia ndani, ambamo namo hamuna mahitaji muhimu kwa maisha. Barabara ni tupu, hospitali haziwezi kufanya kazi na maduka yamekauka bidhaa.

"Watu wanakufa njaa. Madukani hakuna tena kitu, mtu hawezi hata kutoka mtaani, watu wana njaa na kiu. Ikiwa mkasa huu utaendelea kwa wiki moja zaidi, basi litakuwa ni janga." Anasema mkaazi mmoja wa Abobo.

Urusi yapinga mashambulizi dhidi ya Gbagbo

Raia wakikimbia makaazi yao kuhofia mizinga ya vikosi vya Gbagbo na Ouattara
Raia wakikimbia makaazi yao kuhofia mizinga ya vikosi vya Gbagbo na OuattaraPicha: Picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, Urusi imevituhumu vikosi vya Ufaransa na vya walinda amani ya Umoja wa Mataifa vilivyopo Cote d'Ivoire kwa kuingilia kati mgogoro wa ndani wa nchi hiyo na kuegemea upande mmoja, kitendo ambacho inasema kinakiuka sheria za kimataifa.

Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imesema kwamba, inasikitisha kuona kuwa vikosi vya kulinda amani vya kimataifa vinachukua upande katika mgogoro badala ya kuwa katikati, kama ilivyo idhini waliyopewa na Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba, jitihada za sasa za kimataifa za kumuondoa Gbagbo zitamalizikia kwa kukimaliza kipindi cha demokrasia, amani na utangamano nchini Cote d'Ivoire, na badala yake ikataka mataifa ya Afrika yaachiwe wenyewe kuumaliza mgogoro huu.

Lakini Umoja wa Ulaya kwa upande wake, hapo jana ulienda mbali zaidi katika kumshinikiza Gbagbo ajiuzulu, kwa kumbebesha moja kwa moja dhamana ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea nchini humo, hasa kwa wiki mbili zilizopia, ambapo mamia ya watu wamekwishapoteza maisha yao.

Umoja huo umeiomba mahakama ya kimataifa ya uhalifu kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.

Mwandishi: Alexander Göbel/ZPR/AFP/Reuters
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Ramadhani