1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo aonywa na Umoja wa Mataifa

13 Januari 2011

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemuonya upya kiongozi wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wanajeshi 3 wa Umoja wa Mataifa kufyatuliwa risasi na kujeruhiwa na wanajeshi wa Gbagbo.

https://p.dw.com/p/QrxG
epa02505311 (FILE) A file photograph dated 25 October 2010 shows Incumbent Ivory Coast president Laurent Gbagbo speaking during an election rally in Abidjan, Ivory Coast, 29 October 2010. The United Nations Human Rights Commission is meeting in Geneva, Switzerland on 23 December 2010 to discuss the crisis in Ivory Coast as international pressure mounts for Laurent Gbagbo to quit the presidency. A European Union travel ban has been imposed on Gbagbo and his wife Simone as he continues to cling to power refusing to recognise his loss in the 2010 elections. EPA/NIC BOTHMA +++(c) dpa - Bildfunk+++
Laurent Gbagbo hataki kuondoka madarakaniPicha: picture alliance / dpa

Vile vile watu wamepigwa marufuku kutoka nje katika kitongoji cha Abobo na eneo jingine linalojulikana kuwa ni ngome ya Alassane Ouattara, anaetambuliwa na jumuiya ya kimataifa kama rais mpya.

Ausschreitungen Elfenbeinküste
Ghasia zilizoripuka AboboPicha: AP

Askaripolisi sita wameuawa katika mapambano mapya yaliyozuka,kati ya vikosi vya Gbagbo na wafuasi wa Ouattara katika kitongoji cha Abobo nje ya mji mkuu Abidjan ambako watu wamepigwa marufuku kutoka nje wakati wa usiku. Mkuu wa majeshi ya Cote d'Ivoire, jemadari Phillipe Mangou alietangaza amri hiyo amesema eneo la Abobo litazingirwa na majeshi yake. Hata vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa havitoruhusiwa kuingia eneo hilo. Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake hasa baada ya kuripotiwa kuwa majeshi ya Gbagbo yamepanga operesheni mpya katika eneo la Abobo.

Ghasia mpya zazusha hofu

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikosi tiifu vya Gbagbo vinajaribu kuwatimua wanajeshi na polisi wa Umoja wa Mataifa wanaowalinda raia katika eneo hilo. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema, mashambulio yo yote dhidi ya vikosi vyake vya amani ni jambo lisilokubalika. Wahusika watawajibishwa kwa vitendo vyao. Katibu Mkuu Ban Ki-moon, ana wasiwasi pia kuhusu ripoti za machafuko yanayotokea katika maeneo mengine nchini Cote d'Ivoire na amelaani vitendo vyote vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Kommissarin der Vereinten Nationen für Menschenrechte Navi Pillay
Navi Pillay amelaani mauaji ya raiaPicha: AP

Nae mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, hii leo akilaani mauaji ya raia na shambulio lililofanywa dhidi ya vikosi vya amani, nchini Cote d'Ivoire, amearifu kuwa kumegunduliwa kaburi jingine liliokuwa na hadi maiti 80. Inasemekana kuwa kaburi hilo lipo Issia karibu na mji wa Daloa, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa hawakuruhusiwa kwenda huko.

Pillay pia ana wasiwasi kwa vile hadi sasa, hakuna suluhisho la kisiasa lililopatikana kati ya Gbagbo na Ouattara anaetambuliwa na Umoja wa Mataifa kama mshindi wa uchaguzi uliofanywa Novemba mwaka jana. Lakini Gbagbo, anaeungwa mkono na Mahakama Kuu na akidhibiti vikosi vya usalama, amekataa kuondoka madarakani.

Zaidi ya watu 200 wameuawa katika machafuko yaliyotokea katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi huku ikihofiwa kuwa mgogoro huo utashika kasi.Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 25,000 wamekimbilia nchi jirani Liberia.

Mwandishi: Martin,Prema/Reuters
Mpitiaji: Abdul-Rahman