1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA:Haniya azitaka nchi za kiarabu kugomea mkutano unaodhaminiwa na Marekani

7 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Hw

Kiongozi wa serikali ya Hamas huko Gaza Ismail Haniya amezitaka nchi za kiarabu kuususia mkutano wa amani ya mashariki ya kati unaodhaminiwa na Marekani utakaofanyika mwezi ujao.

Katika mahojiano yaliyochapishwa kwenye gazeti moja linalounga mkono kundi la Hamas,Haniya amezitaka Saudi Arabia na Misri kutafakari upya uamuzi wa kushiriki mkutano huo akisema hatarajii mkutano huo kupata mafanikio yoyote.

Matamshi hayo ya Haniya yametolewa kabla ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolezza Rice katika eneo hilo wiki ijayo inayolenga kuongeza nguvu maandalizi ya mkutano huo ambao haujajulikana utafanyika wapi na tarehe ngapi.

Kundi la Hamas liliutwaa ukanda wa Gaza mnamo mwezi Juni na kuvitimua vikosi vya rais Mahmoud Abbas.Hamas ni kundi linaloangaliwa na Marekani,Umoja wa Ulaya na Israel kama kundi la kigaidi kwa sababu ya kukataa kukomesha matumizi ya nguvu dhidi ya taifa la kiyahudi la Israel na pia kukataa kulitambua taifa hilo na kuheshimu makubaliano ya amani yalifikiwa siku za nyuma.