1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Wapalestina watano wauwawa

29 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCWd

Wapalestina watano wameuwawa usiku wa kuamkia leo kwenye machafuko yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza. Idadi ya vifo iliyosababishwa na mapigano kati ya chama cha Hamas na Fatah huko Gaza sasa imefikia watu 30.

Mapigano yameendelea usiku kucha katika mji wa kusini wa Khan Yunis ambako watu watatu waliuwawa. Watu wengine wawili waliuwawa mjini Gaza.

Msemaji wa serikali ya Hamas, Ghazi Hamad, amesema wanazungumza na viongozi wa Fatah kumaliza mapigano. Mapigano hayo yamekwamisha juhudi za kuunda serikali ya umoja wa taifa na kuliweka eneo la Gaza katika hatari ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati huo huo, mfalme Abdullah wa Saudi Arabia amewaalika viongozi wa vyama vya Hamas na Fatah nchini Palestina kwa mazungumzo mjini Makkah.

Kiongozi wa chama tawala cha Hamas aliye uhamishoni, Khaled Meshaal, na kiongozi wa chama cha Fatah, rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, wamesema wako tayari kuhudhuria mazungumzo ya aina hiyo. Hata hivyo tarehe ya mkutano huo haijatangazwa.