1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza- Wajumbe wa Hamas waridhia mpango wa amani wa Misri.

Eric Kalume Ponda14 Januari 2009

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye amewasili mjini Cairo Misri kuanza ziara yake katika eneo la Mashariki ya kati katika juhudi za kuutanzua mzozo wa Gaza,amekariri wito wake wa kusitishwa mashambulizi.

https://p.dw.com/p/GYMt
Wanajeshi wa Israel waimarisha mashambulizi GazaPicha: AP


Pande hizo mbili zimeendelea na mashambulio makali katika barabara za mji wa Gaza huku juhudi za kidiplomasia zikiwa bado hazijafanikiwa baada ya pande hizo kulikataa azimio la umoja wa mataifa la kusitishwa mashambulizi hayo wiki iliyopita.Jee matumaini sasa yanaelekezwa wapi ?


Matumaini sasa yako katika mpango wa amani unaoongozwa na Misri huku kukiwa na hali ya ati ya kuhusu mkutano ulioitishwa na viongozi wa mataifa ya Kiarabu kujadilia mzozo huo mjini Doha Qatar siku ya ijumaa .

Baada kufanya mashauriano na rais wa Misri Hosni Mubarak mjini Cairo, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon alisema kuwa hakuna muda zaidi wa kupoteza katika kusitishwa vita hivyo.


Katibu huyo mkuu alikitaka chama cha Hamas kumomesha mara moja uvumirishwaji wa makombora ya maroketi dhidi ya Israel, huku akiishtumu Israel kwa kutumia nguvu za kijeshi kupita kiasi katika oparesheni zake ndani ya Gaza.


Katibu mkuu huyo alisema baada ya kuchunguza mapendekezo yaliyomo kwenye mpango wa amani unaoongozwa na Misri kwamba anamatumaini mpango huo utafaulu kukomesha mzozo huo, na kuwaepushia dhiki na mateso raia wengi wa Gaza ambao wamekwama katika vita hivyo, akisisitiza haja kwa mataifa ulimwengu kuheshimu maazimio yanayopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa.


Israel leo ilifanya mashambuliomakali ya angani na pia ardhini dhidi ya vituo 60 vya wafuasi wa chama cha Hamas, ambao walijibu kwa makombora matatu yaliyoshambulia mji wa Beersheba kusini mwa Israel.


Wanajeshi wa Israel pia wameshambulia mahandaki 35, ghala 9 za silaha na pia makao makuu ya Polisi wa Hamas katika mji wa Gaza, ambao bado wameuzingira.


Mashambulizi hayo yalitokea karibu na kambi ya wakimbi ya Rafa kwenye mpaka wa Misri na Gaza.Wapiganaji wawili na wanawake wawili waliuawa wakati wa mashambulizi hayo.


Mashirika ya misaada ya binadamu yanasema kuwa hali ni mbaya ndani ya mji huo wa Gaza unaokabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma za kibinadamu.


Wakati huo wajumbe wa chama cha Hamas walifanya mashauriano na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed Aboul Gheit, kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye mpango wa amani unaoongozwa na Misri , ambapo taarifa za hivi punde zinasema sasa chama cha Hamas kimeuridhia.

Habari zaidi zinasema maandalizi ya mkutano wa viongozi wa kiarabu unaotarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa mjini Doha Qatar, bado yanalega lega baada ya kukosa kuungwa mkono na theluthi mbili za mataifa wanachama, idadi inayohitajika kwa Umoja wa nchi za kiarabu kuitisha kikao cha dharura.


Katibu mkuu wa Umoja huo Amr Musa alisema kuwa hadi kufikia sasa ni mataifa 14 wanachama wanaounga mkono mkutano huo kati ya mataifa 15 yanayohitajika kuidhinisha kikao hicho. Umoja wa nchi za Kiarabu wenye mataifa wanachama 22 umegawanyika kuhusiana na mzozo wa Gaza.


Mataifa mawili yenye uwezo mkubwa katika baraza hilo Misri na Saudia Arabia yanapendekeza ajenda hiyo ya Gaza izungumzwe wakati wa mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika kati ya tarehe 19 na 20 mwezi huu


Jumla ya Wapalestina 1,000 wameuawa wakiwemo watoto 292 na wengine zaidi ya 4,000 kujeruhiwa huku Israel ikipoteza wanajeshi 10 na raia watatu tangu vita hivyo vianze huko Gaza disemba 27.


Wakati huo huo serikali ya Lebanon imeshutumu vikali shambulio la kombora kutokea Lebanon katika mji wa Kiryat Shmona nchini Israel,ikikitaja kitendo hicho kuwa kinachotishia usalama wake na sababu ya Israel kuishambulia Lebanon.


Waziri wa habari nchini humo Tarek Mitri alisema kuwa Lebanon kamwe haipasi kuingizwa katika vita vinavyoendelea Gaza.Shambulio hili ni la pili kutekelezwa kutoka upande wa Lebanon tangu wiki iliyopita.