1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza- Israel Wanajeshi wa Israel waendelea kuondoka Gaza.

Eric Kalume Ponda19 Januari 2009

Hali ya utulivu inaendelea kudumishwa katika eneo la Ukanda wa Gaza siku mbili baada ya Israel kutangaza kusimamishwa mapigano na wafuasi wa Chama cha Hamas ambacho pia kimetangaza hatua sawa na hiyo .

https://p.dw.com/p/GbIX
Wanajeshi wa Israel wakionyesha ishara ya ushindi waondoka Gaza.Picha: AP


Wanajeshi wa Israel wanaendelea kuondoka katika ardhi Gaza huku raia wengi wa eneo hilo walinusurika mashambulio hayo wakirejea katika makaazi yao yaliyoharibiwa kabisa.



Maafisa wa Polisi wa Gaza kwa mara ya kwanza tangu vita hivyo vianze disemba 27 walionekana katika barabara za mji wa Gaza wakiwa wamevalia mavazi ya raia baada ya wanajeshi hao wa Israel kuanza kuondoka mji huo.


Wakaazi waliojawa na huzuni na nyuso za kukata tamaa kwa ushirikiano na maafisa wa huduma za binadamu waliendelea kupekua vifusi vya nyumba zilizobomolewa, ambapo maiti za watu 95 zikiwa ni pamoja na watoto ziliondolewa kutoka vifusi hivyo. Katika jengo moja jumla ya maiti 23.


Hadi kufikia sasa zaidi Wapalestina 1,300 wameuawa na wengine 5000 kujeruhiwa. Hali kadhalika ripoti ya hivi punde inasema kuwa zaidi na majengo 4,000 yameharibiwa kabisa ikiwa ni pamoja na mioundo msingi wa eneo hilo la Gaza.


Viongozi wa mataifa ya Magharibi wanasema kuwa kiasi cha dala bilioni 1.6 zitahitajika kujenga upya eneo hilo la Gaza.


Ujumbe wa vionngozi kutoka mataifa ya Magharibi waliohudhuria kikao maalum baada ya kuafikiwa kwa mkataba huo huko Sharm El Sheikh nchini Misri walipongeza hatua hiyo wakisema kuwa ni mwelekeo ufaao wa kupatikana kwa amani ya kudumu katika kanda hiyo.


Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown aliihimiza Israel kufungua maeneo yake ya mpakano ili kutoa nafasi ya misaada zaidi ya kibinadamu.

Brown alisema, ``Naamini kwamba wakati Obama anapoingia madarakani na kuanza kazi, ni wajibu wetu, barala la Ulaya likiliwakilishwa hapa na Itali, Ujerumani, Uhispania Tchekoslovakia na Ufaransa, sote tuliopo hapa siku ya leo, tunawajibu wa kudumisha na kuendelea msingi wa amani ulioanzishwa na Rais Hosni Mubaral ili kuafikia amani ya kudumu na kutambuliwa kwa taifa la Israel na uthabitiwa Wapalestina na kuungwa mkono na mataifa 57 ambayo yanasema yataitambua Israel´´.


Waziri huyo mkuu aliandamana na rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy, na Kansela wa Ujerumani Ngela Merkel.

Ili kuhakikisha mpango huo unadumishwa, Kansela wa Ujerumani Bibi Merkel alisema kuwa Bara la ulaya ambalo limeshirikiana kwa karibu na Misri kufikiwa kwa muafaka huo, litaendelea kutoa msaada wake kuhakikisha udumishwaji wa amani katika eneo hilo la mashariki ya Kati..


alisema Bibi Merkel, ``Ni imani yetu kabla ya kuwapo na uhakika uingizaji wa silaha kutoka nje kupitia mipakani, ama kupitia baharini ni lazima udhibitiwe. Na msaada gani unaweza kupatikana kutoka kamaya ufundi hilo tungependa kulishughulikia´´.


Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert alisema kuwa Israel ilifikia malengo yake ya kupunguza uwezo wa kijeshi wa chama cha Hamas ingawa alisisitza kuwa nchi yake haitasita kujibu mashambulizi yoyote ya mizinga ya maroketi kutoka Gaza. Israel ilipoteza wanajeshi wake 10 na raia watatu wakati wa mapigano hayo yaliyoanza Disemba 27.