1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Allan Johnston aachiliwa huru

4 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBm1

Kundi la wanamgambo la Hamas limesema mwandishi wa habari wa shirika la habari la BBC raia wa Uingereza Allan Johnston ameachiliwa huru.

Johnston amekabidhiwa kwa kundi la Hamas na watekaji nyara wa kundi la Army of Islam waliokuwa wakimuzuilia tangu tarehe 12 mwezi Machi mwaka huu katika Ukanda wa Gaza.

Duru zinasema mwandishi huyo yuko katika hali nzuri kiafya na sasa yumo mikononi mwa maafisa wa kundi la Hamas linalotawala eneo la Ukanda wa Gaza.

Johnston, mwandishi wa habari pekee kutoka mataifa ya magharibi anayefanya kazi katika eneo hilo, alitekwa nyara na kundi la Army of Islam lililo na mafungamano na kundi la al-Qaeda.

Kundi hilo lilitoa picha katika mtandao wa internet likitaka wanamgambo wa kiislamu wanaozuiliwa kwenye magereza nchini Uingereza na nchi nyengine waachiliwe huru.

Tisho la maafisa wa Hamas kutaka kumuokoa Allan Johnston kutumia nguvu lilisababisha kundi hilo kutoa picha zilizomuonyesha akiwa amevaa ukanda wa mabomu na kutishia kumuua ikiwa Hamas ingevamia.