1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gari la Mandela lilishika moto, asema daktari wake

Iddi Ssessanga
17 Julai 2017

Gari la wagonjwa lililombeba rais wa kwanza aliechaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini Nelson Mandela lilishika moto wakati likimkimbiza hospitali, amefichua daktari wake katika kitabu kilichochapishwa Jumatatu.

https://p.dw.com/p/2ggKw
Trauer Mandela Südafrika
Picha: Reuters

Tukio hilo ni mmoja ya vioja vilivyomo katika kitabu hicho kinachoangazia  miaka ya mwisho ya maisha ya Mandela kilichoandikwa na Vejay Ramlakan, ambaye alikuwa daktari mkuu wa upasuaji nchini Afrika Kusini na daktari binafsi wa rais huyo wa zamani hadi alipofariki dunia mwaka 2013.

Ramlakan alikuwa akimsindikiza Mandela kutoka nyumbani kwake mjini Johannesburg kwenda hospitali maalumu ya moyo mjini Pretoria Juni 2013, wakati moshi ulipoanza kufuka kutoka gari la wagonjwa lililokuwa limembeba kiongozi huyo wa zamani wa ukombozi.

"Moshi mzito ulilifunika gari wakati lilipopunguza mwendo na kusimama kwenye njia kuu ," aliandika Ramlakan. " Niliangalia mbele na kuona kile kilichoonekana kama gari lililokuwa linawaka moto... Hili lilikuwa tukio la kuogofya. Madiba katika gari la wagonjwa linalowaka moto," aliongeza Ramlakan, akitumia jina la ukoo la Mandela.

Trauer Mandela Südafrika Paris Eiffelturm
Mnara wa Eifel uliwashwa katika rangi za Afrika Kusini katika kumkubumbuka Mandela.Picha: Reuters

Licha ya hofu ya timu ya madaktari wa Mandela, mgonjwa wao hakudhurika na baada ya dakika 30 alihamishiwa katika gari lingine na kukamilisha safari. Ramlakan pia alifichua kuwa muda mfupi baada ya kifo cha Mandela akiwa na umri wa miaka 95 Desemba 2013 kufuatia maambuzi ya muda mrefu ya mapafu, kamera ya ujasusi ilikutwa katika chumba cha maiti ulipokuwa mwili wake.

Mwaka 2011, kamera tatu za uchunguzi zilizokuwa zinarekodi matukio ya nyumbani kwa Mandela na makaburi ya familia ziligundulika karibu na Qunu, kijiji alikozaliwa Mandela katika mkoa wa Cape ya Mashariki, umbali wa kilomita 450 kusini-mashariki mwa Durban, aliandika Ramlakan.

Kitabu hicho kilichopewa kichwa cha "Miaka ya mwisho ya Mandela" kimetolewa kuelekea siku ya kimataifa ya Mandela, inayoadhimishwa kila mwaka kumkumbuka mpiganiaji huyo wa uhuru na usawa nchini Afrika Kusini na ulimwenguni kote.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Yusuf Saumu