1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi aujia juu Umoja wa Mataifa

2 Machi 2011

Baada ya Umoja wa Mataifa kuisimamisha Libya uwanachama wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja huo, leo Muammar Gaddafi amehutubia mkutano wa kisiasa mjini Tripoli na kurudia msimamo wake wa kutoondoka madarakani.

https://p.dw.com/p/10SOG
Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: dapd

Ikilinganishwa na hotuba yake ya wiki moja nyuma, leo Muammar Gaddafi amezungumza kwa utulivu zaidi. Akijaribu kupangua shutuma dhidi yake, kuanzia ile ya mauaji dhidi ya waandamanaji, ambao umekuwa msingi wa uamuzi wa Umoja wa Mataifa kusimamisha uwanachama wa nchi yake kwenye Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja huo, hadi uwezekano wa kuvamiwa kijeshi, Gaddafi ametumia muda wa karibuni dakika tisiini, kueleza msimamo wa utawala wake.

Kuhusu kusimamishwa uanachama, Gaddafi ameuita uamuzi wa Umoja wa Mataifa, kama usio wa busara na ambao uliongozwa na taarifa zisizo za kweli.

Akarejelea wito uliotolewa hivi karibuni na mtoto wake, Saif al-Islam, wa kuitaka yenyewe jumuiya ya kimataifa ipeleke wachunguzi nchini Libya, kufahamu ukweli halisi ulivyo.

"Wanasema eti Gaddafi anayapa silaha makundi na kuua watu wake. Anawapiga risasi. Mimi nawapenda na napendwa na watu wangu. Hapa hakuna kundi lenye silaha kama Darfur. Nawaje basi kuchunguza wagundue hasa ukweli ni nini". Amesema Gaddafi.

Maandamano ya kumpinga Gaddafi
Maandamano ya kumpinga GaddafiPicha: dapd

Gaddafi amesema, ni bahati mbaya sana kuwa heshima ya nchi yake hivi sasa inahatarishwa na makundi ya kigaidi yanayoongozwa na tawi la Al Qaida la Kaskazini mwa Afrika. Amefikia umbali wa kutoa changamoto kwa wapinzani wake, kama kweli wapo, wajitokeze wazi kuzungumza naye:

"Niko tayari kujadiliana na yeyote kati yao, amiri wao, au mtu yeyote ajichaguwe mwenyewe, aje ajadiliane nami. Lakini hawa hawataki majadiliano, kwa sababu hawana matakwa yoyote, zaidi ya kuua tu." Amesema Gaddafi.

Huku akikatizwa mara kwa mara na wafuasi wake waliohudhuria mkutano huo, ambao walikuwa wakiimba: "Tunakutaka wewe tu Muammar!", Gaddafi amewaonya Walibya, kamwe wasiruhusu uingiliaji kati wa jumuiya ya kimataifa, hasa Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi, NATO, maana utasababisha vifo vya maelfu ya watu, kama inavyotokea sasa Iraq na Afghanistan.

Hata hivyo, amewahakikishia Walibya kuwa, visima vya mafuta viko salama na kwamba jeshi la umma linavilinda, licha ya makundi aliyoita ya kihuni yanayotaka kuvishikilia.

Lakini wakati huo huo akatishia kuihaulisha kwa makampuni ya Kichina biashara yote ya mafuta iliyo kwenye makampuni ya Kimagharibi. Libya huzalisha mapipa milioni moja na nusu ya mafuta kwa siku na kiasi ya asilimia 85 ya mafuta hayo husafirishwa nchi za Ulaya.

Gaddafi ametumia mkutano huu pia kukanusha vikali taarifa kwamba yeye, au familia yake, wanamiliki mali na akaunti za benki nje ya nchi, ambazo kwa siku za karibuni mataifa kadhaa ya Magharibi yamekuwa yakitangaza kuzizuia, akiziita kuwa hizo ni mali za umma wa Libya, na si zake. Kwa mujibu wa mtandao wa WikiLeaks, utajiri wa nje wa Libya unafikia dola za Kimarekani bilioni 32.

Wakati Gaddafi anahutubia mjini Tripoli, taarifa kutoka miji mengine ya nchi hiyo, hasa ya eneo la Mashariki zinaonesha kuwa eneo kubwa limeendelea kubakia mikononi mwa waasi, licha ya jitihada za vikosi vyake kutaka kulirejesha.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman