1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi aadhimisha miaka 40 madarakani

Kabogo Grace Patricia1 Septemba 2009

Madaraka hayo aliyapata baada ya kufanya mapinduzi yasiomwaga damu

https://p.dw.com/p/JNGU
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: AP/Montage DW

Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi leo ameadhimisha miaka 40 alipotwaa madaraka katika mapinduzi yasiomwaga damu -sherehe ambazo zimehudhuriwa na viongozi kutoka Afrika, nchi za Kiarabu na Latin Amerika. Hata hivyo nchi za Magharibi zimezipuuza sherehe hizo.

Shamrashamra za maadhimisho hayo zilianza usiku wa jana katika ngome ya zamani ya jeshi la Marekani huko Matega, karibu na mji mkuu wa Libya, Tripoli. Viongozi walioalikwa na Kanali Gaddafi kuhudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, viongozi wa nchi za kiafrika ambao kabla ya hapo walihudhuria mkutano wa siku moja wa Umoja wa Afrika mjini humo, Rais wa Venezuela Hugo Chavez, Leonel Fernandez wa Jamhuri ya Dominica, Boris Tadic wa Serbia na Rais Gloria Arroyo wa Philippines.

Ratiba ya maadhimisho hayo ya siku nne ni pamoja na gwaride kubwa la kijeshi linalowajumuisha wanajeshi wa Afrika, nchi za kiarabu na Ulaya.

Gaddafi ambaye aliwahi kujielezea kama kiongozi wa viongozi wa nchi za Kiarabu, mfalme wa wafalme wa Afrika na Imam wa Waislam, aliwaalika viongozi wa nchi za Ulaya, ambao hata hivyo hawajahudhuria maadhimisho hayo. Uhusiano wa Libya na nchi za Magharibi umeongezeka kidogo, lakini mwezi uliopita uhusiano huo uliingia dosari baada ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini kumpokea kishujaa mtu aliyepatikana na hatia ya mauaji ya abiria 270 wa ndege ya Marekani ya Pan Am huko Lockerbie, Scotland. Marekani ilionya kuwa mapokezi hayo ya Abdelbaset Ali al-Megrahi, yangevuruga uhusiano ambao umekuwa ukiimarika tangu Libya ilipoacha mpango wake wa kuwa na silaha za maangamizi mwaka 2003.

Kanali Gaddafi, aliyemuondoa madarakani Mfalme Idriss, mwaka 1969 amekaa madarakani kwa muda mrefu.

Aidha, Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limemtaka Kanali Gaddafi kuadhimisha sherehe hizo kwa kuzifuta sheria zote za ukandamizaji pamoja na kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa nchini humo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri: M. Abdul-Rahman