G8 wamtaka Saleh wa Yemen kuondoka madarakani | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.05.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

G8 wamtaka Saleh wa Yemen kuondoka madarakani

Mkutano wa nchi nane zilizoendelea kiviwanda duniani (G8) umeanza huko mjini Deauville, Ufaransa, huku hali ya Yemen na nafasi ya ukuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yakiwa masuala yanayotanda mazungumzo.

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy

Tangu mwanzo suala la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu lilikuwa moja ya ajenda muhimu ya mkutano huu, lakini kubadilika kwa hali ya mambo nchini Yemen, kumeifanya ajenda hii kuwa muhimu zaidi kuliko ilivyopangwa.

Karibu kila kiongozi anayezungumza hadi sasa, anatoa wito kwa Rais Ali Abdullah Saleh kuondoka madarakani, ili kuepusha nchi yake isiingie kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwenyeji wa mkutano huo, Ufaransa, imesema kwamba, Rais Saleh ndiye anayestahiki kulaumiwa kwa mapigano yaliyotokea usiku wa jana, kwa kuwa alikataa kusaini makubaliano yaliyotayarishwa na Baraza la Ushirikano la Nchi za Ghuba, GCC, yanayotaka kuanzishwa kwa serikali ya mpito.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton

Hata Marekani ambayo kwa kawaida ni mshirika mkubwa wa Rais Saleh, kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton imekwenda umbali ambao haujawahi kufikiwa hapo mwanzoni.

"Tunaunga mkono kuondoka kwa Rais Saleh, ambaye kila mara amekuwa akikubali kuondoka madarakani, lakini hatimaye huyakhalifu makubaliano hayo." Amesema Clinton.

Japan nayo, ambayo kwa kawaida ni nchi pekee ndani ya kundi hili la mataifa nane inayojizuia kujihusisha na siasa za mataifa mengine, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, Satoru Satoh, alimtaka Rais Saleh kusaini makubaliano ya kuondoka madarakani aliyoafikiana na wapinzani wake kupitia upatanishi wa GCC.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amesema kwamba mkutano huu unapaswa kuwaonesha watu katika ulimwengu wa Kiarabu kwamba uko pamoja nao.

"Ninataka mkutano hu utowe ujumbe mwepesi na wa wazi, ambao ni kuwa mataifa yenye nguvu kubwa kabisa duniani yamekuja pamoja na yanawaambia wale wanaotaka demokrasia na katika Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, 'tuko pamoja nanyi.' Amesema Cameron.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Kabla ya kuondoka kuelekea Deauville, asubuhi ya leo Kansela wa Ujerumani aliliarifu Bunge kuhusu kile ambacho Ujerumani itakisamamia kwenye mkutano huu.

"Tunakutana katika wakati ambao kuna wimbi la mageuzi Arabuni na Afrika ya Kaskazini, nasi tunapaswa kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu hali hii. Serikali za huko zinajikuta zikilazimika kuakisi matakwa ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ya watu wao." Merkel aliliambia Bunge la Ujerumani asubuhi ya leo.

Mkutano huu unatarajiwa pia kufunikwa na suala la mrithi wa ukuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Mfaransa Dominique Strauss-Kahn, kujiuzulu akikabiliwa na kesi ya ubakaji nchini Marekani.

Wanachama wa Ulaya katika kundi la G8, nchi za Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Italia, wanatafuta uungwaji mkono wa Marekani, Urusi, Canada na Japan, ili mgombea wao, ambaye ni waziri wa sasa fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, apite kwenye nafasi hiyo.

China, ambayo si mwanachama wa kundi la G8 lakini ni taifa lenye usemi mkubwa katika uchumi wa ulimwengu, linatilia shaka chaguo hili la Ulaya, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, akisema kuwa nchi yake haijakuwa na msimamo rasmi kuhusu Lagarde, japokuwa baadhi ya viongozi wa serikali yake wameonesha kumuunga mkono mgombea huyo, ambaye kama atachaguliwa, atakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

 • Tarehe 26.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11OhM
 • Tarehe 26.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11OhM

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com