1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fundisho kwa kanisa katoliki

Maja Dreyer8 Januari 2007

Baada ya askofu ya Warsaw Stanislaw Wielgus kujiuzulu kutokana na kukiri kwamba alishirikiana na idara za ujasusi za zamani za kikomunisti, kanisa la kikatoloki la Poland linapata shida kubwa ya kuaminika. Sababu yake ni kwamba kanisa hili lilionekana kama ishara ya upinzani dhidi ya mfumo wa kikomunisti.

https://p.dw.com/p/CHU2

Tunaanza na maoni yaliyoandikwa katika gazeti la “Frankfurter Neue Presse”:
“Kujiuzulu kulikuwa njia ya pekee. Huenda inaweza kufahamika kwa mtu kushirikiana na idara za ujasusi ikiwa ameshurutishwa. Lakini viwango vya kukisia tabia ya askofu viko juu kuliko kwa watu wa kawaida. Juu ya hayo, kanisa la kikatoliki lilitoa mchango muhimu katika kupindua mamlaka ya wakomunisti. Iwapo askofu alikuwa mpelelezi wa Wakomunisti katika nchi hiyo, basi kanisa litapotea uaminifu wake. Na kwa kanisa, uaminifu ndio msingi mkuu wake.”

Gazeti la “Schwäbische Zeitung” la mjini Leutkirch linaangalia jukumu la Vatikan katika suala hilo na kusema:
“Mchango wa Vatikan katika suala hili hauwezi kutambulika. Inasemekana kuwa Askofu Wielgus aliongea wazi historia yake akizungumza na Pope Benedikt 16. Je, bado alificha mambo fulani? Au labda Vatikan ilijua yote na hata hivyo kumunga mkono askofu huyu? Kwa vyovyote vile, Pope Benedikt anaonekana kwa sura mbaya: Ama hana mamlaka juu ya kanisa lake, ama alikubali kuficha historia hiyo mbaya.”

Tukiendelea zaidi na mada hiyo, sasa ni gazeti la “Lausitzer Rundschau” kutoka mjini Cottbus, kule mpakani mwa Ujerumani na Poland, ambalo limeandika yafuatayo:
“Sasa basi ni Poland ambapo Pope Benedikt wa Ujerumani alishindwa alipojaribu kuficha historia. Hatua ya askofu huyu ya kujiuzulu ni sawa, kwa sababu cheo hiki muhimu cha askofu wa Warsaw hakifai kuchukuliwa na mtu aliyekuwa na mabwana wawili. Kwa Benedikt 16. ni fundisho gumu, na pia kwa kanisa zima la katoliki ni fundisho la kwamba kanisa pia linahusishwa na mizozo ya kijamii.”

Na tunakamilisha udondozi huu wa magazeti tukilinukuu gazeti la “Sächsische Zeitung” kutoka mji wa Dresden ulioko pia katika eneo la Mashariki mwa Ujerumani. Gazeti hili limeandika:
“Kinyume na Ujerumani ambapo mabaki ya idara za ujasusi za Serikali ya zamani ya kikomunisti yalijadiliwa wazi, nchini Poland utaratibu wa kufichua kazi za idara za ujasusi ulianza miaka michache tu iliyopita. Katika utaratibu huu kanisa liliwekwa kando na kutohusishwa na mjadala huu kuhusu historia ya kikomunisti. Lakini hii haiwezekani. Mjadala huu mkali baada ya askofu Wielgus kujiuzulu unaonyesha kiti kimoja, yaani kupasuka kwa jamii hakuweza kuzuiliwa kwa kuficha ukweli."