1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Frof. Zibakalam atunukiwa tuzo ya Uhuru wa habari

Sekione Kitojo
3 Mei 2018

Mtaalamu wa masuala ya siasa wa Iran Sadegh Zibakalam atunukiwa tuzo ya uhuru wa kutoa maoni. Mahojiano yake na DW, yanamuweka hatarini kukabiliwa na adhabu ya kifungo.

https://p.dw.com/p/2x77g
Iran Sadegh Zibakalam, Politologe
Picha: Isna

Profesa  Zibakalam  hii  sio  mara  ya  kwanza kuingia  matatani na serikali . Na kutokana na ujasiri  wake wa kuikosoa serikali  ya  Iran  Zibakalam ametunukiwa  tuzo ya uhuru wa kutoa maoni uhuru wa vyombo vya habari.

"Nafikiri  kosa  langu  ni kwamba  katika  mahojiano  na  DW nilizungumzia  kuhusu  masuala  ya  kisiasa, mawazo  ambayo  serikali inayapinga", amesema  Sadegh Zibakalam. Wakati  serikali  ikisema, kwamba  machafuko  nchini  Iran yanatokana  na  maadui  wa  nchi hiyo, serikali  inatarajia, kwamba  kila  mmoja  atafuata  msimamo  huo na  kuurudia."

Prof. Sadegh Zibakalam
Sadegh Zibakalam mtaalamu wa masuala ya siasa katika chuo kikuu mjini TehranPicha: DW

Sadegh zibakalam  hajafanya  hivyo. Mwezi  Januari  alisema  mtaalamu huyo  wa  masuala  ya  siasa  kutoka  Iran  katika  mahojiano  na  DW idhaa  ya  Kifarsi  kuhusiana  na  hali  ya  machafuko  wakati  ule  nchini Iran.

Wakati  huo  Wairan  zaidi  ya  10,000  waliingia  mtaani , wakipinga sera  za  kiuchumi  pamoja  na  uongozi  mzima  wa  kisiasa  nchini humo. Zibakalam  alionesha  kuwaelewa  waandamanaji  pamoja  na kupinga  shutuma  za  serikali. "Nasema , kwamba  maandamano yalipangwa  na  kuongozwa  na  Wairan wenyewe. Na  hakuna  kabisa mtu  yeyote  kutoka  nje  ya  Iran aliingiza  ushawishi  wake. Kwa  kweli hakuna  ushawishi  wa  nje  katika   maandamano  hayo",  alisema Zibakalam  katika mahojiano  na  DW. Kutokana  na  hayo  Zibakalam mwenye  umri  wa  miaka  69 anakabiliwa  na  kifungo  cha  miaka  18.

Zibakalam kutengwa kijamii

Mwezi  Machi mahakama  ya  serikali  ya  mapinduzi  ya  Iran  ilitoa hukumu  hiyo  dhidi  ya  Zibakalam. Iwapo  itathibitishwa, mtaalamu huyo  wa  kisiasa  hatafungwa  tu  jela, lakini  pia atakabiliwa  na adhabu  ya  miaka  miwili  ya kutengwa kijamii.  Hii  ina  maana , Zibakalam  hataweza  kufanya  mahojiano  na  chombo  chochote  cha habari , na  hataweza  kuandika makala  yoyote kwa  umma.

Bildergalerie Presse Iran KW 46
Maeonesho ya vyombo vya habari mjini Tehran. Mchoro wa kuchekesha unaomuonesha mtaalamu huyo ZibakalamPicha: Isna

Na  pia hataruhusiwa  kutumia  mitandao  ya  kijamii  kwa  muda  wa miaka  miwili. Zibakalam  amekata  rufaa  dhidi  ya  hukumu  hiyo, hata hivyo uamuzi  bado  haujachukuliwa.  Hadi wakati  huo atakaa  kimya, kujilinda?  Kwa  Zibakalam  inaonekana  kwamba  hilo sio  njia anayoitaka. Adhabu  hiyo  inayomkabili  hamshughulishi  mtaalamu  huyo wa  masuala  ya  siasa,  na  kila  siku  yuko  katika  ukurasa  wa  Twitter na  Facebook  na  kutoa  maneno  ya  ukosoaji  wa  wazi.

"Wakati mahakama  itakaponiambia : Profesa  Zibakalam, huruhusiwi  kufanya mahojiano  tena,  hapo  ndio  nitaacha.  Lakini  hilo  hawajalifanya. Ndio sababu  nasubiri   hadi  sasa,  hadi  pale  mahakama  ya  rufaa itakapotoa  uamuzi  wao," amesema  hayo   katika  mahojiano  na  DW.

Mhalifu sugu

Kwa  upande  wa  mahakama  nchini  Iran  Zibakalam  ni  mhalifu anayerejea  uhalifu  kila  mara. Profesa  huyo  wa  chuo  kikuu  cha mjini  Tehran  ni  mmoja  kati  ya  wasomi  maarufu  na  wataalamu  wa siasa  nchini  Iran. Zibakalam ni  mmoja  kati  ya  watu  waliomo  katika kundi  la  wanamageuzi  walioko  karibu  na  rais Hassan Rouhani.

Bildergalerie Iran KW 46 Zibakalam
Profesa Zibakalam katika mjadalaPicha: Tasnim

Anafahamika  kwa  jinsi  anavyoweza  kuendesha  majadiliano   akiwa na  msimamo  mkali. Na  pia  amekuwa  akiikosoa  serikali  katika  sera zake  za  siasa  za  nje  na  pia  misimamo  ya  serikali. Mwezi  Februari 2014  aliwahi  kusema, kuhusu kuitambua  Israel  kama  taifa  na  pia Marekani. Zibakalam amekuwa  mwanafunzi  katika  chuo  kikuu  cha masuala  ya  kisiasa   nchini  Uingereza  cha  Brandford. Katika maandishi  yake  aliandika  kuhusu "mapinduzi  ya  Kiislamu na  siasa za  mataifa  ya  magharibi".

Wakati  akiwa  mwanafunzi   mwaka  1974  alitembelea  nchini  mwake na  kukamatwa  na  askari  kanzu  wa  Shah, kutokana  na  kuihujumu nchi  pamoja  na  kutoa  propaganda. Baada  ya  mapinduzi  ya Kiislamu  alirejea  nyumbani  mwanzoni  mwa  miaka  ya  1980. Miaka michache  baadaye  alianza  kazi  yake  katika  chuo  kikuu  cha  Iran mjini  Tehran. Mwaka  2000  aligombea  katika  uchaguzi  wa  bunge nchini  Iran  katika  mji  wa  Zanjan  kaskazini  magharibi  mwa  Iran. Hata  hivyo  hakuruhusiwa  kugombea na  baraza  la  kuchuja wagombea  la  taifa.

Mwandishi: Rahel klein / ZR / Sekione Kitojo

Mahriri: Mohammed Abdul-Rahman