1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Finali ya Kombe la Asia:Irak dhidi ya saudi Arabia

Ramadhan Ali27 Julai 2007

Endapo kombe la Asia kesho likinyakuliwa na Iraq ,mashabiki bila kujali madhehebu yao-wsasuni au washia au hata wakurdi,wanapanga kusherehekea pamoja kama wairaki.

https://p.dw.com/p/CHbY

Kesho ni finali ya Kombe la Asia kati ya Iraq na Saudi Arabia.Mashabiki wa dimba wa Iraq wanasema hawajali tofauti zao iwapo ni washia,wasuni au wakurdi.Kwa pamoja kama juzi walipoitimua Korea ya kusini mabao 4-3 kuingia finali wanapanga shamra-shamra mjini Baghdad,Basra na Kirkuk.Iwapo Iraq italinyanyua kombe kesho,basi itakua “asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu ende Baghdad.”

Miripuko 2 ya mabomu iliolengwa kundi la mashabiki waliokuwa wakisherehekea juzi ushindi dhidi ya korea ya Kusini wa mabao 4-3 iliua si chini ya mashabiki 51 wa Irak na kuwajeruhi wengine 126.

Kuna mashabiki ambao kesho watajitolea mhanga maisha yao na kuingia barabarani kuadhimisha ushindi,kwani wanasema kuwa, muhimu kwao ni kuonesha umoja wa wairaki.

“Tutajitolea mhanga na kutojali kufa tukipepea bendera ya Iraq na kuwaambia wauaji na wanasiasakuwa,tumeungana kitu kimoja.”-alisema Abdul-Hussein Khazal Obeid.

Lakini, sio mashabiki wote watakaojitolea mhamnga.Kuna wengine wanaosema kwamba, watasherehekea nyumbani.Mmoja wao ni Mateen Omar Khorsheed wa kabila la Turkman.

Akalaumu hujuma iliotokea majuzi mjini Baghdad pale mashabiki waliposhangiria ushindi wa mabao 4-3 wa Irak dhidi ya Korea ya kusini.

“kilichotokea Baghdad ni kisa kinachotoa mfano mbaya.Kwani, mashabiki waliosherehekea mitaani hawakufanya vile kwa niaba ya madhehebu yao,bali walishangiria kwa niaba ya Iraq.”-alisema Khorsheed.

Ni katika hali hii timu ya taifa ya Iraq chini ya kocha mbrazil, ndio inaingia kesho uwanjani dhidi ya jirani Saudi Arabia,mabingwa mara kadhaa wa kombela Asia.

Iraq itamtegemea tena nahodha wake Younis Mahmoud, aliekosea mara mbili kutia bao katika nusu-finali ya majuzi na Korea ya Kusini.

Mwengine, anaetazamiwa kutamba ni mchezaji wao wa kiungo Karrar Jassim.

Timu ya Irak imefanya maajabu makubwa kufika finali ya kesho ya Asian Cup-kwani njiani mabingwa wengi wa zamani wameanguka na sio tu Korea ya Kusini,bali hata Japan na Iran.Australia ilioshiriki mara ya kwanza katika kombe hili pia haikufua dafu.

Timu ya Irak ilijiandaa nje ya Irak.Ikicheza nchi jirani ya Jordan na wakati mwengine katika viwanja vya Iraq ya kaskazini kwa wakaurdi kwenye usalama kidogo.Kwahivyo, ni ajabu katika masharti kama hayo, Iraq imetamba na kufika finali.

Saudi Arabia ina ajenda nyengine hapo kesho.Kwani baada ya msukosuko waliopata katika kombe lililopita la Asia huko China 2004,wasaudi wamepania kuridi kesho na kombe mjini Riyadh.Saudi Arabia ilitolewa katika duru ya kwanza tu ya Kombe lililopita la Asia.

Katika mji mtakatifu wa Karbala,Sheikh Aqil Abid Salim, anaiombea dua timu ya Irak iwike kesho.Wakati huo huo lakini, analaani jinsi mashabiki walivyoshangiria ushindi wa jumatatu dhidi ya korea ya Kusini ulioikatia tikiti ya finali .

Anasema ,“kufyatua risasi hewani,kucheza ngoma barabarani na kuvua nguo, hakulingani kabisa na ustaarabu na mila za wairaqi.”

Juu ya hivyo, ikiwa Iraq itondoka na kombe kesho,Shiekh Salman na wanazuoni wenzake wa kishia,watabidi kufumba macho na kuvumilia duru nyengine ya shangwe n a shamra shamra-kwani Kombe la Asia,limewasili Baghdad.