1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FINALI YA KOMBE LA AFRIKA

8 Februari 2008

Ghana wenyeji wanacheza leo na Ivory Coast kuania nafasi ya 3 wakati mabingwa Misri wana miadi kesho Accra na simba wa nyika.

https://p.dw.com/p/D4ab

Kesho (jumapili) itajulikana wapi kombe la 26 la Afrika litaelekea .Litarudi Misri au simba wa nyika watavaa taji lao la 5.

Jioni hii (jumamosi)-wenyeji Ghana wanaumana na tembo wa ivory Coast kufuta machozi ya kupigwa kumbo timu zote mbili nje ya finali ya kesho mjini Accra zikiania nafasi ya 3.

Rais Thabo Mbeki alikanusha jana kwamba msukosuko wa umeme nchini unaweza ukaathiri maandalio ya Kombe la dunia 2010 na kesho timu 2 za kileleni katika Bundesliga-Munich na Bremen zaumana.

Mabingwa wa Afrika Misri wana yakini sana kutamba kwa mara ya pili katika kombe hili la 26 la Afrika hapo kesho mjini Accra mbele ya simba wa nyika-Kamerun na kuvaa taji kwa mara ya 6 ikiwa ni historia.

Misri –mabingwa waliizaba Kamerun mabao 4-2 katika duru yao ya kwanza walipokutana nchini ghana wiki kiasi 3 zilizopita na kama wasemavyo wahenga-mramba asali-harambi mara moja.

Misri iliwachezesha Tembo wa Ivory Coast na nahodha wao Didier Drogba kindumbwendumbwe charira huko Kumasi hapo juzi na kuwatimua nje kwa mabao 4:1 la Abdelader keita.

Ufunguo wa ushindi wa mabingwa dhidi ya Ivory Coast walikuwa nao mastadi3:Nyuma alikuwa kipa wao essam Al Hadari alieokoa mabao kadhaa ambayo akina Drogba na Keita wakivurumisha langoni mwake.Usoni alikuwa Ahmed Fathi alievunja tumbuu ya lango la Ivory Coast mnamo dakika ya 12 ya mchezo-bao hilo lilifungua wazi ngome ya Corte d’Iviore,kwavile Tembo walibidi kutia fora usoni kurejesha bao.

Halafu Amr Zaki akalifumania lango la Tembo wakati wakihemkwa usoni mwa lango la Misri kujaribu kusawazisha.Kwa mabao yake 2 kila baada ya dakika 5 za kipindi cha pili, Amr Zaki aliwazika Tembo kaburini mjini Kumasi.Bao la Abdekader keita lililofanya matokeo 2:1 likafutwa na mabao ya Zaki.Msumari wa mwisho katika jeneza la Tembo ukakomelewa mnamo dakika ya 90 ya mchezo na Aboutreika baada ya pasi maridadi kutoka kwa Mohamed Zidan.

Katika nusu-finali ya pili iliotangulia hii kati ya misri na Corte d’iviore, simba wa nyika Kamerun ambao walikwishatolewa maanani kwamba hawangenguruma tena katika kombe hili la Afrika baada ya kuaibishwa na Misri,waliwasangaza wenyeji Ghana kwa kuondoka na ushindi wa bao 1:0 mjini Accra.Kamerun mabingwa mara 4 wa Afrika ,kwanza 1984 mjini Abidjan, 1988,2000 na 2002,ilitamba kufuatia bao maridadi la Alain Nkong ambae akiichezea timu ya taifa kwa mara ya pili tu.Pasi maridadi kutoka Samuel Eto’o ilimuona Nkong akifyatuka na mpira kwa kasi na kuusindikiza katika lango la Ghana.

Kama ilivyobashiriwa,jahazi bila ya nahodha wake,huenda mrama:na Ghana ikicheza bila John Mensah kati ya uwanja ,iliyumbayumba.Michael Essien alierithi unahodha kutoka kwa Mensah ,hakufua dafu siku hiyo.

Kocha mfaransa Claude Le Roy akimuweka kando nje ya uwanja Asamoah Gyan, chaguo lake la akina Laryea Kingston na Junior Agogo halikuvunja gogo.

Kocha wa Kamerun,mjerumani Otto Fpfister,aliegonga mno vichwa vya habari wiki hiii huko Ghana , alitoa kielezo hiki kwanini Black Stzars-nyota yao ilishindwa kunawiri juzi katika mawingu ya Accra:

Alitoa jukumu la kushindwa Ghana mabegani mwa vyombo vyake vya habari kwa sehemu mmoja.Alidai Fpister, magazeti ya ghana kabla mpambano yakiandika kuwa Ghana italibeba kombe hapo kesho jumapili.yalichosahau magazeti hayo-asema Otto Pfister, kabla hujabeba kombe inakupasa kwanza kucheza dimba.hii ndio maana yeye asema hapendi kuagua na kuhanikiza atashinda.Tukicheza kesho bora kuliko maadui zetu-alisema Otto basi tutakuwa na nafasi ya kushinda.Ikiwa hatutacheza uzuri ,basi hatutashinda. Huo ndio wasia wake kocha husu wa kijerumani wa simba wa nyika.

Jioni hii lakini timu 2 zilizotolewa nje ya finali-wenyeji Ghana na majirani zao Ivory Coast wanarudi uwanjani mara hii kuania nani anamaliza nafasi ya 3 na kutwaa medali ya shaba nyuma ya Misri au Kamerun .

Kesho sio tu hatima ya kombe la Afrika la mataifa 2008 itaamuliwa mjini Accra, huenda pia hatima ya timu gani itaudhibiti barabara kileleni usukani wa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani:

Bayern Munich iliopo nafasi ya kwanza katika ngazi ya Ligi inapambana kesho na Werder Bremen iliopo nafasi ya pili.

Bayern inaongoza Ligi kwa pointi 3 wakati Bremen itahitaji ushindi kufuta mwanya huo wa pointi 3.

Munich lakini itabidi kesho kucheza bila ya stadi wake wa Ufaransa Franck Ribery.Isitoshe, iliwahi munich kuongoza Ligi hii kwa pointi 6 kati ya Oktoba na X-masi, kufanya madhambi tena yaweza ikaadhibiwa.

Bremen ilifanya uzembe jumamosi iliopita ilipozabwa nyumbani na timu chipukizi ya Bochum mabao 2:1.Inahitaji kwahivyo, pointi 3 kesho kwa kila hali kuweka hesabu sawa.ikishinda kesho Munich itarudi kufungua mwanya wa pointi 6 kilelelni kati yake na Bremen.

Mpambano mwengine wa kukata na shoka kesho ni ule baina ya schalke na Borussia Dortmund.Schalke iko nafasi ya 5 ya ngazi ya Ligi na wanajua mpambano na mahasimu wao wa mtaani Dortmund si mteremko.Kwahivyo, mashabiki wa Bundesliga wanaosubiri pia mastadi wao kadhaa kurejea wiki ijayo Ujerumani kutoka kombe la Afrika ,wanasubiri kwa shauku kubwa changamoto za kesho tangu huko Accra hata mjini Munich.