1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Finali :Ujerumani na Spain

27 Juni 2008

Finali ya kombe la ulaya jumapili hii itakua kati ya Ujerumani na Spian.Spain iliilaza jana Russia 3:0.

https://p.dw.com/p/ERwE

Kwa ushindi wa jana wa mabao 3:0 dhidi ya Russia,Spain ina miadi jumapili hii na Ujerumani kuamua nani kati yao ataibuka bingwa wa kombe la ulaya la 2008.Spian iliitoa hapo kabla Itali-mabingwa wa dunia ambao jana wamemtimua kocha wao Roberto Donadoni na kumrejesha yule wa zamani aliewaongoza kutwaa kombe la dunia 2006 hapa Ujerumani, Marcello Lippi.

Barabara za jiji kuu la Spian -Madrid jana usiku lilijionea fiesta-shangwe na shamra shamra,lakini haikua tu Madrid,bali takriban kote Spina -kuanzia Barcelona hadi Mallorca.

Waspain walianza taratibu,lakini kilipoanza kipindi cha pili, walitia kasi na hii iliwapatia mabao 3-la kwanza likiwa la Xavi Hernandez,lapili Daniel Guiza na la 3 lililopiga msumari wa mwisho katika jeneza la warusi alipachika David Silva.

Spian sasa ina miadi na Ujerumani kwa jumapili hii na ilicheza finali yake ya mwisho ya kombe hili miaka 24 iliopita , 1984 na kulazwa na wenyeji Ufaransa chini ya usukani wa Michel Platini,leo rais wa UEFA.

Aliechochea moto katika lango la warusi si mwengine bali chipukizi Fabregas,kijana aliechapa ule mkwaju wa penalty ulioitoa Itali nje ya kombe hili.

Fabregas -mshambulizi wa Arsenal London,aliitwa mnamo dakika ya 34 ya mchezo kujaza pengo la la David Villa alieumia.Villa-mshambulizi wa Valencia, ndie anaeongoza orodha ya watiaji mabao mengi katika kombe hili:4,akifuatwa na mjerumani Lucas Podolski.Fabregas ndie aliekua ufunguo wa ushindi wa Spian tena hapo jana.

Kocha wa Russia,Guus Hiddink alieipiga kumbo nchi yake Holland, baada ya mchezo alisema:

"Tumeshindwa na timu kali sana.Spian ni timu nzuri sana."

Spain, ikijiandaa kukutana na Ujerumani jumapili hii, kocha wa Ujerumani Joachim Loew,alisema jana kwamba amevutiwa mno na mchezo wa Spain .Akaongeza, "Spain ilitamba kweli na wamecheza kwa hali ya juu mechi zao zote."