1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Figo na Praag wajiondoa katika uchaguzi wa urais wa FIFA

22 Mei 2015

Luis Figo na Michael van Praag wamejiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha urais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Alhamis wiki hii. Uchaguzi huo utafanyika Me 29

https://p.dw.com/p/1FURQ
FIFA Präsidentschaft Kandidaten Luis Figo Michael van Praag
Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Kujiondoa kwa wagombea hao kumemuacha mwanamfalme wa Jordan Ali Bin Al Hussein kuwa mgombea pekee atakayepambana na rais wa sasa na mtu ambaye anaonekana kuwa huenda akashinda Sepp Blatter.

Blatter mwenye umri wa miaka 79, anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa ataibuka mshindi kwa kipindi cha tano hapo Mei 29, hata kama , chini ya uangalizi wake FIFA imetumbukia katika wimbi la kashfa na utata.

Fußball FIFA Joseph S. Blatter
Sepp Blatter anawania muhula wa tano uongoziniPicha: picture-alliance/dpa/A. Sultan

Haya ni pamoja na madai ya rushwa katika mchakato wa kupata nchi zitakazokuwa wenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2018 na 2022 hadi mzozo kuhusiana na saa zenye thamani ya dola 25,000 kila moja zilizotolewa zawadi kwa wajumbe wa kamati ya utendaji katika kombe la dunia mwaka jana.

UEFA ikiwa na kura 53 kati ya kura 209 katika uchaguzi , imesema haitamuunga mkono Blatter, lakini raia huyo wa Uswisi ameahidiwa uungwaji mkono mkubwa kutoka vyama vingine duniani kote.

Rais wa shirikisho la kandanda la Uholanzi Michael van Praag ameamua kumuunga mkono mwanamfalme Ali , akisema kwamba amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina na kushauriana na pande mbali mbali zinazohusika pamoja na wadau mbali mbali.

Fifa-Vizepräsident Prinz Ali bin al-Hussein
Ali Bin al Hussein apatambana na Blatter katika uchaguziPicha: picture alliance/Pressefoto Ulmer

Ninafuraha tele mahali nilipo sasa. Lakini nahisi kwamba FIFA inahitaji kufanya vizuri zaidi na kwamba si rahisi kwamba FIFA inasonga mbele ikiwa na uongozi wake wa sasa. Ndio maana nimeamua kugombea dhidi ya Blatter. Tunahitaji mabadiliko katika utawala, uongozi na utamaduni wa FIFA. Tunahitaji kukumbatia ukosoaji kama motisha ya kufanya vizuri zaidi.

Kwa pamoja wagombea hao dhidi ya Sepp Blatter wameona kwamba mmoja mmoja hawawezi kumwangusha Blatter na hivyo ni lazima waungane ili kuweza kumuondoa madarakani Sepp Blatter.

Kampeni hii ilikuwa wakati wote juu ya haja ya kulipeleka soka mbele na kuiimarisha FIFA na bado nia hiyo ipo. Ndio sababu sisi watatu tulikaa pamoja na kujadili nafasi zetu. Nina ungwa mkono na nchi nyingi za Ulaya na nyingi nyingine duniani kote. Kama sisi sote. Kwa hiyo tumeamua kuweka karata zetu pamoja mezani. Kwasababu pia tuliamua kwamba tunaamini, kama ilivyo kwa wadau wengine muhimu duniani, kwamba mgombea mmoja atakuwa na nafasi kubwa kushinda uchaguzi huu. Mwanamfalme Ali Al Hussein ameweza kuonesha hivyo, kwamba katika wakati huu, yeye ndie mgombea ambaye ana nafasi kubwa kupambana na Sepp Blatter.

Joseph Blatter anawania muhula wa tano madarakani katika FIFA kama rais lakini anakabiliwa na upinzani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002 katika uchaguzi utakaofanyika Mei 29.

Blatter anaendelea kuwa mgombea anayeonekana kuwa atashinda wakati mwanamfalme Ali anaahidi utawala bora lakini pia fedha zaidi kwa wanachama wa FIFA.

Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef