1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ferguson na ziara ya Papa Strassbourg Magazetini

26 Novemba 2014

Ziara fupi ya kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis katika taasisi za Umoja wa Ulaya mjini Strasbourg na maandamano ya Ferguson ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/1Dtu9
Maandamano dhidi ya uamuzi wa jopo la wanasheria wa Ferguson yamefika pia Los AngelesPicha: Reuters/M. Anzuoni

Tuanzie lakini na kilio kilichohanikiza nchini Marekani kulalamika dhidi ya uamuzi wa jopo la wanasheria unaoondowa uwezekano wa kufikishwa mahakamani askari polisi wa kizungu Darren Wilson aliyempiga risasi na kumuuwa,mmarekani mweusi, kijana wa miaka 18 Michael Brown,msimu wa kiangazi uliopita.Maandamano hayo yaliyoripuka jumatatu yameenea katika miji tofauti ya Marekani.Gazeti la "Landeszeitung" linaandika kuhusu matumaini yaliyofifia ya kuona hali ya mambo ikibadilika baada ya rais wa kwanza mwesi kuingia madarakani huko White House.Gazeti linaendelea kuandika:

Januari 20 mwaka 2009 ilidhihirika kana kwamba mambo yatabadilika na kila kitu kitakuwa bora.Kwasababu wakati ule ,Barack Obama aliingia madarakani akiwa rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya kiafrika.Lakini mpaka leo hii hakuna ishara inayoonyesha kwamba dhana mbaya zilizoenea katika majimbo mengi ya Marekani za wazungu dhidi ya wamarekani weusi au kinyume chake, zimetoweka.Machafuko ya Ferguson ambayo ni jibu kwa uamuzi unaomtaja polisi wa kizungu kuwa hana hatia,mtu aliweza kutabiri yatatokea.Anaejidai kushtuka,hataki tu kuutambua ukweli wa mambo.Na ukweli huo ni kwamba idadi ya wamarekani weusi vijana waliouliwa wakati wa malumbano na polisi ni kubwa mno ikilinganisahwa na idadi ya wenzao wa kizungu.Mwakilishi wa halmashauri kuu ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binaadam,ameitolea wito Marekani ichunguze kwa makini madai ya ubaguzi dhidi ya polisi.Amefika hadi ya kuzungumzia kuhusu "ubaguzi unaolindwa kisheria nchini Marekani".Matamshi makali zaidi ya hayo hayajawahi kutolewa dhidi ya nchi inayojinata kuwa kitovu cha demokrasia na ngome ya uvumilifu."

Mwito mkali wa Papa Francis

Ziara fupi iliyofanywa jana na kiongozi wa kanisa katoliki katika taasisi za Umoja wa ulaya katika mji wa Ufaransa wa Strassburg katika jimbo la Alsace nayo pia imegonga vichwa vya habari humu nchini hii leo.Alikuwa na maneno makali kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani dhidi ya Ulaya aliyosema imezama katika bahari ya matatizo ya ndani na kuweka kando sifa zake za "utu."Gazeti la Lübecker Nachrichten" linaandika:

Strasbourg ameutumia tu kama jukwaa la kuufikisha ujumbe wake.Waliokusudiwa hasa lakini wanakutikana katika miji mikuu ya Ulaya.Kwamba hakuna sera za Ulaya kuhusu wakimbizi ,makosa ni ya serikali husika.Zinafanya kila liwezekanalo kuhakikisha idadi ndogo tu ya wakimbizi ndio wanaopokelewa na kwa namna hiyo kupunguza mzigo wa gharama.Idadi kubwa ya nchi zinalifumbia macho tatizo la wakimbizi.Kwa pamoja nchi za Ulaya zinashughulikia zaidi kuhakikisha mipaka ya nje imefungwa.Kwa namna hiyo wanabeba sehemu ya dhamana ya kuzama umati wa watu katika bahari ya Mediterenia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Mohammed Aboul Rahman