1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fedha zaidi zahitajika kuzuwiya kuibuka upya kwa malaria

17 Desemba 2012

Shirila la Afya Duniani WHO Jumatatu (17.12.2012) limeonya kwamba mafanikio ya kupiga vita malaria yanaweza kuvurugwa venginevyo wafadhili wanakubali kutumia fedha zaidi katika kinga dhidi na katika kuutibu ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/173z4
Malaria
Malaria

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema katika repoti yake hiyo kwamba serikali za nchi zinazoathirika na ugonjwa huo na mataifa fadhili ziliongeza michango yao ya fedha katika kupambana na ugonjwa huo kati ya mwaka 2004 na mwaka 2009 lakini michango hiyo ikaja kupunguwa baada ya hapo.Juu ya kwamba zaidi ya vifo vya watu milioni moja kutokana na malaria vilizuiliwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kutokana na mipango maalum ya afya , zaidi ya watu 600,000 bado wanaendelea kupoteza maisha yao kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.

Zahitajika hatua za haraka

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Margaret Chan amesema lazima wachukuwe hatua kwa haraka na kwa dhamira kuzuwiya kuponyokwa na mafanikio makubwa ambayo tayari wameyapata katika kuupiga vita ugonjwa huo. Kwa mujibu wa Chan mtoto wa Kiafrika anakufa kila baada ya dakika moja kutokana na malaria.Inabidi zitumike dola bilioni 5.1 kwa mwaka kufikia mwaka 2020 ili kuzuwiya na kutibu malaria katika nchi 99 zilizoathirika na ugonjwa huo .Mwaka jana zilipatikana dola bilioni 2.3 tu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)Margaret Chan.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)Margaret Chan.Picha: AP

Ugonjwa wa malaria unasababishwa na mbu na unaweza kuzuiliwa kabisa na kutibiwa. Idadi ya vyanduruwa vilivyonyunyuziwa madawa ya kuuwa mbu ambavyo hutolewa kwa watu wanaoishi kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika imepunguwa sana katika kipindi cha miezi 24 iliopita.WHO imeonya kwamba hali hiyo yumkini ikapelekea kuibuka upya kwa ugonjwam huo.Juhudi za kunyunyiza madawa ya kuuwa mbu majumbani barani Afrika pia zimekuwa zikisuasua.

Tiba ya ufanisi inahitajika

Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni nchi ambazo zimeathirika sana na ugonjwa huo wakati India ni nchi ilioathirika zaidi barani Asia.WHO pia imesema kwamba tiba ya ugonjwa huo inapaswa kutolewa kwa ufanisi zaidi.Kwa mujibu wa repoti ya WHO Barani Afrika watu wengi hupatiwa madawa bila ya kufanyiwa uchunguzi ipasavyo wa ugonjwa huo.Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia ambaye ni Mwenyekiti wa Muungano wa Kupiga Vita Malaria wa Viongozi wa Afrika pia ameizindua repoti hiyo mjini Monrovia leo hii ambapo ametowa wito wa kuendelezwa kwa juhudi za kupiga vita ugonjwa huo na kufanya kila liwezakanalo kuzuwiya kuibuka upya kwa ugonjwa huo.

Matumizi ya vyandarua ni muhimu kudhibiti malaria.
Matumizi ya vyandarua ni muhimu kudhibiti malaria.Picha: Edlena Barros

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa

Mhariri: Josephat Charo